"TSHISHIMBI" MWINGINE AJA YANGA SC

MASHABIKI wa Yanga wameonjeshwa uhondo wa kiungo mwenye mambo mengi uwanjani Papy Kabamba Tshishimbi ambaye amekuwa gumzo kila kona kutokana na vitu vyake.

Hata hivyo, uhondo huo wa Tshishimbi ukiwa haujapoa,uongozi wa klabu hiyo umemleta mtu mwingine mwenye uwezo mkubwa kama yeye, ingawa anacheza nafasi tofauti.

Safari hii anayekuja ni bonge la beki kisiki atakayekuja kuziba nafasi ya Mtogo Vincent Bossou aliyetemwa.
Tshishimbi ambaye ni raia wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo aliyenunuliwa na Yanga akitokea Mbabane Swalloows ya Swaziland, amewahakikishia mabosi hao kuwa kama beki huyo atataua na kushirikiana vizuri na waliopo, hao mastraika wanaoogopwa akina Emmanuel Okwi hawatafanya lolote.

Habari za uhakika zinadai kwamba mchezaji huyo alifikia hatua hiyo baada ya kuona aina ya wachezaji wa timu za Simba na Lipuli walizovaana nazo.

Yanga inahaha kusaka beki wa kati wa kuziba nafasi ya Mtogo Vincent Bossou aliyemaliza mkataba, baada ya kushindwa kufanya usajili mpya dakika za mwishoni kutokana na kubanwa na kanuni za Ligi Kuu Bara.

Taarifa kutoka ndani ya mabosi wa Yanga ni kwamba Tshishimbi amewakabidhi jina la beki anayemwamini kwamba ataweza kutuliza ukuta wao ambao kwa sasa upo chini ya Andrew Vincent, Donte, Kelvin Yondani na Nadir Haroubu ‘Kandavaro’.

Saluti5 imejiridhisha kwamba viongozi hao wamepewa jina la beki huyo na muda wowote wataanzisha mazungumzo naye kwa ajili ya usajili wa  dirisha dogo linalofunguliwa Novemba hadi Desemba.

Mtu mmoja wa karibu na Tshishimbi amemkariri kiungo huyo akisema ni kweli wamefanya naye mazungomzo na kukubaliana aje kujiunga na Yanga wakati wowote katika kipindi cha usajili cha dirisha dogo.

Imeelezwa kuwa beki huyo ni Mkongomani na ni rafiki mkubwa wa Tshishimbi ingawa walikuwa hawachezi timu moja na kwamba akija atawadhibiti sana mastraika
Ingawa hakuna kiongozi aliyekuwa tayari kuanika jina la beki huyo lakini imebainika kuwa ni mmoja kati ya marafiki wa karibu na Tshishimbi aliyekuwa akicheza soka katika klabu ya Mbabane Higranders ya Swaziland akijulikana kwa jina la Kingu Penga.


Naye mmoja katika mabosi wa Yanga alisema “Tuliamua kumuuliza Tshishimbi kama anaweza kumjua mchezaji yeyote anayeweza kutufanyia kazi safu yetu ya ulinzi hasa beki wa kati.”

No comments