TSHISHIMBI: OBREY CHIRWA NI MTAMBO WA MABAO YANGA

KIUNGO wa Yanga, Papii Tshishimbi amemuangalia mshambuliaji Obrey Chirwa na vitu vyake katika mazoezi kisha akasema kuwa sasa mwenye kazi yake amerudi na kwamba mtambo wa mabao umerejea.

Tshishimbi amesema amemuona Chirwa tangu aanze mazoezi na kwamba mshambuliaji huyo raia wa Zambia ni mtu anayeijua kazi yake na sasa wapinzani watamkoma.

Tshishimbi raia wa DRC Congo alisema Chirwa ni aina ya washambuliaji wabishi, anayetaka kila wakati kumuingiza beki katika boksi ili afanye makosa, jambo ambalo walikuwa wakimkosa mtu wa namna hiyo katika safu yao ya ushambuliaji.

Alisema Chirwa amechelewa kurudi kutoka katika hali ya majeruhi na kwamba endapo angekuwepo katika mchezo dhidi ya Simba na hata mechi ya kwanza ya Ligi, basi wanachama na wapenzi wa Yanga wangekuwa na furaha kubwa kwa sasa.

“Nimemuona Chirwa, huyu kweli mshambuliaji, naweza kusema sasa kuna kitu kimeongezeka chenye ubora katika safu yetu ya ushambuliaji, nimemkubali sana,” alisema Tshishimbi.  


“Unajua tulikuwa tunamkosa mtu atakayefanya mabeki wa upinzani wafanye makosa, sasa huyu Chirwa hakubali kushindwa kwa mabeki kirahisi, ni mbishi na ana kasi, tungempata mapema hata Simba na wale tulioanza nao Ligi wasingetoka salama, sasa ngoja atafute kasi, akianza kufunga tu itakuwa hatari sana.”

No comments