WENGER ASEMA HANA MASHAKA NA MSIMAMO WA SANCHEZ

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amemkingia kifua mshambuliaji wake Alexis Sanchez na kusema hana mashaka kuwa nyota huyo atarejea kwenye makali yake.
Sanchez, 28, alikaribia sana kuhamia Manchester City dakika za mwisho, lakini Wenger amesema "hana shaka kuhusu fikira na msimamo wa Alexis".
Arsenal walikuwa wamekubaliana uhamisho wake wa £60m na City lakini ilitegemea iwapo wangefanikiwa kumpata Thomas Lemar, ambaye aliamua kusalia Monaco.
"Atarejea upesi sana kucheza katika kiwango chake kizuri kabisa," amesema Mfaransa huyo.
"Soko limefungwa kwa sasa, kulikuwa na mambo mengi sana yaliyokuwa yanaendelea. Ni vigumu sana kuzungumza kuhusu hilo kwa sababu Lemar sasa yuko Monaco na lazima aangazie kucheza huko, Sanchez yuko hapa na anaangazia hapa," Wenger ameongeza
Arsenal walianza ligi kwa ushindi wa 4-3 nyumbani dhidi ya Leicester, kabla ya kushindwa 1-0 Stoke na 4-0 Liverpool, kichapo ambacho kilimuuma sana Wenger.
Mechi yao ijayo itakuwa Jumamosi nyumbani dhidi ya Bournemouth saa 11 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

No comments