YANGA YAMWONGEZEA KANDARASI PAPY KABAMBA TSHISHIMBI

UONGOZI wa Yanga umepiga hesabu ndefu na kuamua kufanya maamuzi ya maana baada ya kufikia kumuongezea mkataba zaidi kiungo wao, Papy Tshishimbi.

Taarifa kutoka kamati ya usajili ya Yanga ni kwamba akili ya haraka iliyopigwa ni pale mkataba wa miaka miwili utakapomalizika haraka ambapo kiungo huyo anaweza kuleta ugumu kusaini mkataba mpya.

Bosi mmoja wa Yanga amesema kuwa wanachofanya sasa ni kuangalia mapema kumuongezea mkataba mrefu kiungo huyo ambaye makocha wengi wameanza kunusa kwamba hatadumu muda mrefu ambapo anaweza kuuzwa nje wakati wowote.

Bosi huyo alisema kuwa tayari kiungo mwenyewe ameanza kuonyesha dalili ya kukubali mawazo hayo ambapo sasa anayesubiriwa ni mwenyekiti wa kamati ya usajili, Hussein Nyika aliyeko safarini nchini Uganda kuanza mchakato huo.

“Unajua tunaona jinsi mikataba ya miaka miwili inavyokuwa mifupi, hasa kwa wale wachezaji wanaoonekana kuwa na ubora mkubwa. Kupitia hilo, ndio maana tumeanza kuliangalia upya hili la Tshishimbi,” alisema bosi huyo.


“Tumeshaanza kumgusia mchezaji mwenyewe juu ya hilo na ameshaanza kuonyesha kwamba hana tatizo, anachotaka ni maslahi mazuri, jambo ambalo liko ndani ya uwezo wetu.”

No comments