ALLY MAYAI TEMBELE ASEMA KICHUYA AMENG'ARA MCHEZO WA LEO

MCHAMBUZI wa mchezo wa soka, Ally Mayai Tembele amemiminia sifa kemkemu mchezaji wa Simba, Shiza Ramadhani Kichuya akisema kuwa ameonyesha ukomavu mkubwa katika kipute cha leo cha watani wa jadi, Simba na Yanga kilichopigwa kwenye dimba la Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Mayai amesema kuwa wakati Kichuya alipokuwa akiitumikia Mtibwa Sugar ya Manungu, Morogoro, alikuwa anasimama kama winga kibendera ambapo sasa amebadilika na kugeuka kuwa kiungo fundi wa kisasa mwenye madhara makubwa kwa wapinzani.

Akitoa uchambuzi wake kupitia azam tv baada ya mchezo huo, alisema bao lililofungwa na mchezaji huyo katika dakika ya 57, lilitokana zaidi na uzembe wa mabeki wa timu ya Yanga, hasa kwa kukosa umakini wa kuusoma mchezo.

Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 baada ya mshambuliaji obrey chirwa kuisawazishia yanga dakika tatu baada ya bao la kichuya.

Baadhi ya mashabiki wa Yanga walioohojiwa na runinga ya Azam Tv wameonyesha kufurahia sare ya bao 1-1 walioipata dhidi ya mahasimu wao, Simba SC, huku wadau wengi wa soka wakiponda kitendo hicho na kudai kuwa kinadhihirisha waliwahofia mahasimu wao hao tangu kabla.

Hata hivyo, Ally Mayai ambaye ni mmoja wa mchambuzi wa soka Tanzania, amesema kuwa Yanga walipaswa kujiuliza badala ya kufurahia sare hiyo ambayo amesema hata hivyo kwa upande wao haiwaongezei chochote.

No comments