ATHUMAN MACHUPA AIPA DARASA SIMBA SC

SIMBA wanaongoza Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara na kuonekana wako vizuri, lakini kama kweli wanataka kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara wanatakiwa kukomaa na kila mechi iliyoko mbele yao.

Hayo ni maoni ya mshambuliaji wa zamani wa Wekundu hao, Athuman Machupa ambaye amesema kwamba usajili ambao Simba umeifanya ni mzuri lakini wanatakiwa kucheza na nidhamu wakati wote hadi mwishoni mwa Ligi kwasababu Ligi Kuu ina ushindani mkubwa.

“Watu wasiibeze Yanga na kuiondoa kwenye nafasi ya kugombania ubingwa kwa sababu bado wapo kwenye nafasi nzuri lakini Simba wamesajili vizuri na hadi sasa wanaongoza Ligi kitu ambacho kitawapa kujiamini kwa sababu wame-miss ubingwa kwa muda mrefu, kuongoza kwao Ligi kutawaweka kuwa tayari kwa kila mchezo,” amesema Machupa.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa timu ya taifa pia “Taifa Stars” ametaja timu anazodhani zitamaliza katika nafasi za nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ni Simba, Yanga, Singida United na Azam.

“Ukiangalia mwenendo wa Ligi Kuu mpaka sasa inaonyesha timu zimejiandaa vizuri, tunaweza tukaona viwango vizuri zaidi na nimeshtushwa kuwaona Singida wapo pale kutokana uzoefu tulionao kuhusu timu zinazopanda kucheza Ligi Kuu.

Machupa amesema kwamba anaona kuna mabadiliko kwenye Ligi na angependa kuona kiwango cha soka la Tanzania kinapanda lakini kuanzia kwenye ngazi ya vilabu.

“Kwa kawaida Tanzania tumezoea kuona Yanga, Simba na Mtibwa ndio zinapambania Ubingwa lakini mwaka huu inatupa sura kwamba kuna timu nyingi zinaweza kuwania taji la Ligi kama Singida, Azam, Mtibwa, Yanga na Simba," amesema Machupa ambaye baada ya kutamba sana na Simba alikimbilia barani Ulaya katika nchi ya Sweden ambako amechezea vilabu kadhaa.

No comments