AYA 15 ZA SAID MDOE: KIINGILIO KINYWAJI SAWA, LAKINI OFA YA MBEGE NI ZAIDI YA TUSI KWA MUZIKI WA DANSI


Wasomaji wazuri wa alama za nyakati huwa wanasema ukiona mgonjwa mahututi anapiga sana kwikwi basi hiyo si dalili nzuri, kuna harufu ya kifo hapo. Naanza kupata hofu na hizi kwikwi zinazobisha hodi kwenye muziki wa dansi.

Hebu sikia hii!!! Show ya Mapacha Watatu Original kila Jumapili ndani ya Sam Pub, Ubungo Kibo, jijini Dar es Salaam, itakupa vitu viwili kwa mpigo - kwanza utapata fursa ya kuona show bure kabisa bila kiingilio chochote, pili kwa wale watumiaji wa pombe za jadi, watapewa ofa ya mbege. Hii ni zaidi ya kwikwi, dansi letu linajua lenyewe linapoelekea.

Ni kweli kabisa kuwa muziki wa kiingilio kinywaji haukwepeki tena, hali ya uchumi imekuwa ngumu na bendi nyingi zinashindwa kufanya maonyesho ya kiingilio cha pesa, lakini ikifikia hatua ya kutembeza na ofa ya mbege juu yake, inakuwa hakuna tofauti na kwikwi za mgonjwa mahututi.

Sasa hivi ni mwendo wa show za bure, mwenye ukumbi anamaliza kila kitu na kisha mwanamuziki ndiyo anakuwa muhubiri wa kuhimiza wateja waongeze salio la kinywaji mezani.

Zamani kulikuwa na bendi hazikubali kupiga bure hata uwape pesa mara mbili ya bei yao kawaida, kitendo cha kwenda kupiga kwenye bar kwa kiingilio cha kinywaji ilikuwa ni sumu kwao …labda ‘itokee’ tu.

Sasa hivi unaweza ukazitafuta kwa tochi bendi zinazokataa show za kiingilio kinywaji …Ni mwendo wa kusuka au kunyoa – kataa show bure ukose cha kuwalipa wasanii wako au pokea show za bure ili angalau bendi iweze kujikimu.

Siku zote nimekuwa mpinzani mkubwa wa show za bure nikiamini kuwa zinaporomosha muziki wa dansi na taarab, lakini wakati mwingine unalazimika kuwahurumia wamiliki wa bendi kwa hasara kubwa wanazopota kutokana na show za kiingilio cha mlangoni. Ila hili la ofa ya mbege mtanisamehe bure.


Mapromota waliokuwa wakikodi hizi bendi na kupunguza mzigo wa uendeshaji kwa wamiliki wameyeyuka huku sababu kubwa ikiwa ni hasara wanazopata - Kwamba kila promota anayekodi bendi na kuingia gharama kibao, anajikuta akishindwa kurejesha gharama zake, mtaji unapungua siku hadi siku na hatimaye kukata shauri kuwa muziki haulipi tena.

Kutokana na hali hiyo, mzigo wa kuandaa show umerejea kwa wenye bendi, show inaandaliwa kwa gharama ya shilingi laki tano hadi saba, kisha show inaingiza laki nne hadi sita. Hapo ndipo show za bure zinapokuwa hazikwepeki …Mwenye bar anakupa laki sita ambayo haikugharimu chochote katika maandalizi ya show, unaiachaje??

Ukichanganua kwa makini unajikuta huna hatua nyingine ya kufanya zaidi ya kutia kibindoni laki sita na kupunguza mlolongo wa show zako za kiingilio cha mlangoni. Sio siri kuwa show za bure zinatia lawama na aibu lakini mwisho wa siku, unaambiwa heri lawama kuliko fedheha.

Nini kinatakiwa kufanywa na bendi zetu katika kipindi hiki cha mpito? Je zibweteke na show za bure? Hapana hata kidogo …Show za bure ni njia katika moja ya njia za bendi zetu kuelekea ‘kaburini’, ni show za kuogopa kama ukoma kwa sababu hiyo ndiyo hatua ya mwisho kabla bendi haijaitwa marehemu.

Jiulize ni hatua gani itafuata siku mwenye bar akiona hapati tena faida …iko wazi kabisa – atakushusha bei tena na tena, mwisho wa siku atakatisha mkataba. Yakikuta hayo katika bar zote unazozitegemea bendi yako INAKUFA kwa kuwa huna tena uwezo wa kurudi kwenye show za kiingilio.

Bendi hazipaswi kubweteka, zinapaswa kuzichukua show za kiingilio kinywaji kama changamoto na kichocheo cha kujipanga upya, zipige kazi ya nguvu ili kuteka mashabiki wapya watakaothubutu kulipa kiingilio siku ikibidi kufanya hivyo. Kuanza kutafuta ubunifu wa kutangaza ofa za mbege si hatua ya kujikwamua bali ni dalili ya kutapatapa.

Bendi zisikubali kuwa na show zote za bure, zihakikishe zinakuwa na ngome angalau moja kwa wiki ambayo itakuwa ni ya kiingilio cha pesa mlangoni, zifanye hivyo kwa gharama yoyote hata ikibidi kukopa kutoka kwenye kile wanachovuna katika show zao za kiingilio kinywaji. Kutokuwa na ujasiri wa kufanya hivyo ni sawa na kujitanguliza chumba cha wagonjwa mahututi kabla hata hujawa mahututi.

Kitendo cha Mapacha Watatu ya Khalid Chokoraa kutumia ofa ya pombe ya kienyeji (mbege) kama kivutio cha baadhi ya maonyesho yao, ni zaidi ya tusi kwa muziki wa dansi. Ifike wakati tukubali kufa na tai zetu shingoni, mambo mengine tuyaonee aibu kuyatamka.


No comments