AYA 15 ZA SAID MDOE: MUUMIN, NYOSHI, SIKINDE WALISTAHILI KUWEPO TANZANIA BAND FESTIVAL


Kuna  aina ya wanamuziki ambao unaweza kuamini kwa akili zako zote hadi za mvunguni kuwa wamekwisha kisanii, lakini utakapowakaribisha kwenye tamasha kubwa lenye mashabiki wengi, watakuduwaza.

Hawa ni wale wanamuziki waliotukuka,  waliofanikiwa kuweka muhuri kwenye kazi zao kupitia tungo za dhahabu na kuacha kumbukumbu  isiyofutika kwa miaka mingi.

Mchukulie Khadija Kopa kama msanii muhenga, kama msanii ambaye tungo zake za sasa zimeshindwa kufunika kazi zake za zamani, lakini mshirikishe kwenye tamasha lako la halafu ushuhuide vumbi lake – atawafunika wasanii wengi unaoamini kuwa wako kisasa zaidi.

Mchukue Juma Nature ambaye kimafanikio kwasasa kaachwa mbali na wasanii wengi waliomkuta kwenye game, halafu mchanganye nao kwenye tamasha kubwa kisha aimbe moja ya nyimbo zake kali, nakuhakikishia utawasahau mastaa wote wa sasa.

Tanzania Band Festival, tamasha kubwa la muziki wa dansi linafanyika kwa mwaka wa pili, safari hii likiwa limepelekwa hadi mikoani, hadi sasa limeshuhudia bendi tano tu zilizoshiriki – Malaika Band, Twanga Pepeta, Msondo Ngoma, FM Academia na B Band.

Moja ya dosari nilizoziona kwenye maonyesho yaliyofanyika, ni kupooza kwa bendi shiriki, kuishi kindugu sana, kwenda kimya kimya kwenye show kama vile wanasindikiza msiba. Hatujazoea hivyo kwenye dansi.

Naam muziki wa dansi umelala, unahitaji amsha amsha zinazopambwa na wasanii wenye uwezo wa kuteka mashabiki kabla na wakati wa onyesho. malumbano, majigambo na ubora wa kazi ndo mtaji mkuu. Kama ni undugu basi urejee baada ya maonyesho na si vinginevyo.

Na hapo ndipo napoona umuhimu wa mtu kama Mwinyuma Muumin kwenye Tanzania Band Festival, nauona umuhimu wa Nyoshi, naona umuhimu wa bendi ya Mlimani Park “Sikinde Ngoma ya Ukae”.Wakati limefanyika onyesho la Dimba Music Concert pale Travertine Hotel, Magomeni jijini Dar es Salaam, Muumin aliwaduwaza watu walioamini kuwa amekwisha.

Muumin alikuwa wa mwisho kutumbuiza na wakati MC anatangaza kuwa sasa ni zamu ya Muumin, ukumbi mzima ulilipuka makelele ya nguvu, nakiri kuwa wakati akielekea jukwani, Muumin ndiye aliyeshangiliwa kuliko wasanii wote na kama angechagua nyimbo sahihi, basi angeiteka show.

Wanapokutana Sikinde na Msondo ni lazima viibuke vita vya propaganda, lazima yaibuke makundi makubwa ya mashabiki wanaofagilia bendi zao. Kwa hakika zinapokutana jukwaa moja bendi hizi hakuna inayokubali kushindwa na mwenzake. Huwa panachimbika.

Na ukitaka kujua athari ya Sikinde kwa Msondo, angalia namna tangazo la show za Tanzania Band Festival huko mikoani lilivyotengenezwa kimakosa …eti mtangazaji anasikika akisema ‘Msondo Ngoma wana wa Ukae’. Ukiweka neno ‘ukae’ kwa Msondo inakuwa sawa kumpa ‘Dawa Mseto’ mgonjwa wa mafua.

Naangalia namna ambavyo Nyoshi huwa hachagui nani yuko mbele yake katika kutandika madongo, namna ambavyo anajua kujiandaa na show kubwa, jinsi anayojua kujipigia promo, namuona kuwa ni mtu sahihi kuwepo katika Tanzania Band Festival bila kujali angekusanya wasanii gani wa kushirikiana naye.

Uwepo wake ungeamsha upinzani mkali dhidi ya FM Academia na hiyo ingekuwa chachu ya dansi kuzungumzika, Muumin angechokozana na Chocky ni wazi kuwa ingeibua msuguano kati ya Twanga Pepeta na Double M Plus.

Najua bado kuna maonyesho kadhaa ya Tanzania Band Festival yanakuja kabla mwaka huu haujafika ukingoni, waandaaji waangalie aina ya wasanii watakaokuwa mtaji kwenye tamasha lao, wasanii watakaoongeza amsha amsha kabla na wakati wa onyesho.


No comments