Habari

AYA 15 ZA SAID MDOE: NYIMBO MPYA ZA DANSI ZIMEGEUKA KUWA BIDHAA HARAMU

on

Majuzi nilihudhuria onyesho la Tanzania Band Festival pale mjini
Dodoma ambapo bendi tano zilichuana jukwaa moja huku tamasha hilo likipambwa na
ukame wa nyimbo mpya.
Mtu pekee alipiga wimbo wake mpya ni Christian Bella kupitia kibao
chake “Punguza Mikogo” lakini bendi zingine zote zilibebwa na tungo zao zamani.
Nikajiuliza kulikoni? Kwanini bendi haziamini katika nyimbo zao mpya?
Zinashindwa kutoa albam mpya, zinashindwa kutoa hata nyimbo mpya japo moja katika
kila miezi mitatu?
Kuna wakati ilikuwa ni habari ya mjini pale linapokuja suala la bendi
ya muziki wa dansi kuzindua albam mpya.
Jiji la Dar es Salaam lilikuwa linazizima mwezi mzima kuelekea
uzinduzi wa albam, bendi zikaweka kambi ili kujiandaa na tukio hilo muhimu.
Kama vile hiyo haitoshi, mashabiki wa kutupwa kutoka miji mbali mbali
ikiwemo Arusha, Moshi, Tanga na Morogoro, walikuwa wakihakikisha wanafunga
safari kuja Dar es Salaam kushuhudia uzinduzi wa albam za bendi zao.
Vituko vilivyokuwa vikiandamana kwenye uzinduzi wa albam navyo
vilikuwa na ladha ya aina yake, mara Ally Chocky kaingia ukumbini na farasi,
mara siku nyingine aingie na tinga tinga, mara aibukie juu ya paa la ukumbi wa
Diamond Jubilee, mara Banza Stone aingie kama askari mwenye cheo cha juu
(Jenerali).
Muumin aingie na kundi la watu walioigiza kama waganga wa kienyeji,
Badi Bakule aingie na jeneza, ili mradi kila staa wa bendi aliandaliwa kituko
cha kuteka vichwa vya habari vya magazeti.
Ukiachana na mbwembwe hizo, soko la albam ya muziki wa dansi lilikuwa
juu sana miaka ya mwishoni mwa 90 hadi miaka ya 2000.
Wasambazaji wakubwa wa kazi za muziki akina GMC na wengineo
wakazithamini bendi zetu kiasi hata cha kuwapa mikopo ya kununua vyombo, kuweka
kambi au ya kuingia studio kurekodi albam mpya. Hawakuwa na wasiwasi wa
kutolipwa, muziki wa dansi ulikuwa unalipa.
Lakini taratibu mambo yakaanza kubadilika, albam zikaanza kupunguza
umaarufu sokoni, wasambazaji wakaanza kuangalia upepo mwingine, wakachungulia
kwenye taarab na muziki wa injili.
Mbaya zaidi ni kwamba watu wa dansi wameridhika na matokeo na
hawafanyi juhudi zozote za kurejea kwenye ufalme wao, dansi linatoka wodi ya
wagonjwa wa kawaida na kupelewa chumba cha wagonjwa mahututi, mwisho wa siku
muziki wa dansi utaishia kwenye majokofu ya vyumba vya maiti.
Kama tunasema nyimbo za dansi hazipigwi radioni, kama albam haziuziki,
kama wasambazaji hawautaki muziki wa dansi lakini bendi zinaweza kugawa nyimbo
mpya bure hadi kwa whatsapp, kwanini tushindwe kutumia majukwaa makubwa kama ya
Tanzania Band Festival kunadi nyimbo mpya?
Nilidhani angalau basi bendi zingejikita kutoa wimbo mmoja (audio na
video) kila baada ya kipindi fulani na kuufanyia juhudi za makusudi ili uchezwe
kwenye vituo vya radio na televisheni, kwenye mitandao na kwingineko. Hii
maanake nini? Maanake ni kwamba wimbo uking’ara basi ni wazi kuwa mashabiki nao
wataongezeka kwenye kumbi za dansi.
Muziki wa dansi umelala, wanamuziki na wamiliki wa bendi nao
wanajiunga katika usingizi huu mzito kwa ‘kususa’ kutoa nyimbo mpya, kususa
kupiga nyimbo mpya kwenye show zao, wanaamini kuendelea kuhubiri kauli ya
nyimbo za dansi kutopigwa radioni ni kisingizio tosha.
Nyimbo mpya za dansi kwenye maonyesho makubwa zimekuwa ni kama bidhaa
haramu, yaani utadhani bendi zimeambiwa zikipiga nyimbo mpya zitachukuliwa
hatua kali za kisheria.

Comments

comments

About Saluti 5

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *