AYA 15 ZA SAID MDOE: VISINGIZIO NDIO ZETU KWA WA WASANII WETU


Mwaka jana winga wa Argentina Angel Di Maria alifiwa na bibi yake dakika chache kabla ya mchezo dhidi ya Chile katika michuano ya Copa America, lakini bado alicheza mchezo huo na kuwa ‘man of the match’.

Naam alikuwa nyota wa mchezo kwa namna alivyotengeneza nafasi nyingi pamoja na kufunga bao moja katika ushindi wao wa 2-1.

Hamasa iliyowazunguka wachezaji wenzake waliokuwa uwanjani na hata wale waliokuwa benchi ilikuwa ya aina yake na ilisisimua zaidi pale alipofunga na kukimbilia benchi ambako wachezaji wenzake walimpokea kwa kumrushia fulana nyeupe iliyokuwa na maneno ya kufariji juu ya msiba wa bibi (nyanya) yake.

Lakini mara kadhaa tumeshuhudia kwenye michezo mikubwa ya kimataifa mchezaji akipata msiba mkubwa wa mtu wake wa karibu – baba mzazi, mama, dada au kaka, lakini bado wanaendelea na michuano hadi mwisho kabla ya kwenda kuhani msiba. Uwajibikaji ulioje huo!

Najaribu kuvuta picha kwa wanamichezo na wasanii wetu wa Kibongo juu ya hali hiyo, sipati picha kabisa ingekuweje.

Sina kumbukumbu nzuri kwa wanamichezo wa Kibongo juu ya tatizo kama hilo, lakini nimewahi kushuhudia wasanii kibao wakikacha maonyesho ya bendi zao kwasababu tu ya kufiwa na jirani achilia mbali ndugu zao wa karibu.

Nimewahi kushuhudia wasanii wengi wakizisusa bendi zao kwasababu tu walinyimwa ruhusa kwenda kumuuguza ndugu yake wa karibu.

Yaani mgonjwa yupo nyumbani – anaugulia nyumbani kwa muda mrefu tu – msanii anaomba ruhusa siku ya onyesho anakataliwa anaambiwa subiri kesho utaenda, linakuwa kosa, mtu anasusa au kuhama bendi. Madeko yaliyoje hayo!


Dhana ya uwajibikaji wa wasanii wetu iko mbali sana na badala yake uvivu na majungu ndiyo yanayochukua nafasi. Wachache wanaozingatia hilo na kutusua kwenye soko wanabaki wakipewa majina kadha wa kadha. “Anabebwa”, “Mchawi”, “Mhongaji”, ili mradi kila jina baya atatafutiwa.

Niliwahi kusikia kuwa mwimbaji niliyempenda  sana marehemu Shaaban Dede aliwahi kutimuliwa Msondo Ngoma kwasababu tu alitoraka dansi la machana la bendi yake na kwenda Uwanja waTaifa kuangalia mechi ya Simba. Kama ni kweli hiyo nayo ilikuwa aina mbovu ya uwajibikaji.

Siku moja nikiwa kwenye kongamano moja la muziki, mtoa mada (Kelvin Twisa) alizungumzia namna baadhi ya wasanii wa Kitanzania wanavyoshindwa kuendana na dhana ya uwajibikaji.

Twisa akasema kulikwa na onyesho kubwa la J Martin wa Nigeria, mmoja wa wasanii nyota wa Tanzania aliyepaswa kushiriki onyesho hilo akafika eneo la tukio saa nzima baada ya J Martin kuwasili kinyume na makubaliano aliyopewa kwamba yeye anatakiwa kufika kabla ya staa huyo wa Nigeria.

Lakini bado msanii huyo wa nyumbani akamwambia Twisa siwezi kupanda jukwaani bila bangi na kwamba amemwagiza mtu akamchukulie kwa kuwa yeye alikurupuka kuwahi hapo kabla hajapuliza bangi lake.

Hivyo ndivyo ilivyo kwa wasanii wa Kitanzania uwajibikaji kwao ni msamiati mgumu – visingizio ndiyo jadi yao, ubabaishaji ndio sifa yao kuu, majungu ndiyo mtaji wao.

Hawasheshimu muda wa kazi, hawaheshimu eneo lao la kazi, hawaheshimu pesa za mashabiki wao na wala hawaheshimu vipaji vyao.   


No comments