KOCHA WA AZAM AAHIDI KUPANDISHA CHIPUKIZI WENGI ZAIDI KIKOSI CHA WAKUBWA

KOCHA wa timu ya Azam FC, Aristica Cioaba amesema kwamba atahakikisha anaibua makinda wengine katika kikosi cha timu ya wakubwa baada ya kuanza na Paul Peter.

Kocha huyo alimuibua kinda Paul na kumpa nafasi katika kikosi chake cha kwanza kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida United ambapo aliingia akitokea benchi na kufunga bao muhimu la kusawazisha katika mchezo ulioisha kwa sare ya bao 1-1.

“Paul ni mshambuliaji mzuri kijana. Licha ya uchanga wake haikunipa shida kumpa nafasi kwenye mechi iliyopita, angalia alivyoweza kupambana na kutumia nafasi moja aliyoipata kufunga bao muhimu, hili ni jambo zuri kwa klabu kuwa na vijana wa aina ya Paul, nina furaha pia kusikia ameitwa timu ya taifa ya vijana, Ngorongoro Heroes, naamini atawafungulia njia wachezaji wengine wa Azam B kupata nafasi hii kama yeye.”

“Mimi ni kocha ninayependa vijana nimepanga kuendelea na njia hii ya kuwapa hamasa kwa kuwajumuisha timu kubwa. Sitajiuliza ninapoona mchezaji mzuri kwenye timu ya vijana, hasa ninapoona ana uwezo wa kuisaidia timu kubwa, bado kuna zaidi ili niwajumuishe timu ya wakubwa,” aliongeza.


Cioaba amekuwa na mfumo mzuri wa kuwajenga wachezaji vijana na kuwapa nafasi kwenye kikosi chake, mpaka sasa ingizo la Peter linakuwa ni la sita kwenye kikosi cha wakubwa baada ya kuwapa nafasi mshambuliaji Yahya Zayd, Shaaban Idd, viungo Brayson Raphael, Stanslaus Ladislaus na beki wa kulia, Abdul Omary “Hama hama”.

No comments