MBEYA CITY YAPIGANIA USHINDI MECHI ZOTE ZA UWANJA WAO WA NYUMBANI

TIMU ya Mbeya City imepania kuhakikisha inashinda katika michezo yote iliyobakia ambayo itahusisha mechi zinazochezwa katika uwanja wake wa nyumbani, Sokoine.

Meneja wa timu hiyo, Geofrey Katepa amesema kwamba huo ndio mpango wao ambao wamejiwekea msimu huu ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.

“Tunahitaji kushinda kila mchezo katika uwanja wa Sokoine lakini pia tunatazamia kufanya vizuri katika mechi ya ugenini, lakini nyumbani hapana hatutakubali kupoteza hata alama moja,” alisema Meneja huyo.

“Bila kujiwekea malengo ya namna hii hatuwezi kufika popote, zaidi tutaendelea kuwa wasindikizaji jambo ambalo tumeona hapana ushindi lazima uanzie kwenye uwanja wa nyumbani kabla ya kutoka nje,” aliongeza.


Meneja huyo pia alidai walianza vibaya kwenye michuano ya Ligi Kuu kwasababu ya kuchelewa kuanza maandalizi ya msimu mpya lakini sasa tayari kikosi chao kimetengeneza maelewano na kina uwiano mzuri uwanjani.

No comments