MISHI ZELE MGUU MMOJA JAHAZI MGUU MMOJA YAH TMK … ni wiki 2 za maamuzi mazito


Mwimbaji tegemeo wa Jahazi Modern Taarab, Mishi Zele (pichani juu) amewaacha njia panda mashabiki wake baada ya hatma yake kuning’inia baina ya bendi mbili pinzani.

Msanii huyo anayetesa na wimbo wake “Nia Safi Hairogwi” kwasasa anahusishwa kwa nguvu na uhamisho wa kwenda Yah TMK Modern Taarab.

Kwa wiki mbili sasa, Mishi haonekani kwenye jukwaa la Jahazi na badala yake amekuwa akishiriki maonyesho ya kundi la Yah TMK Modern Taarab.

Hapo kabla, Saluti5 ilielezwa kuwa Mishi ni miongoni mwa waimbaji watano waliogoma kazi kwa madai ya kutolipwa stahiki zao.

Waimbaji wengine wanaotajwa katika mpango huo ni Hadija Mbegu, Marim Kasola, Mariam BSS na Mwanaidi Ramadhani.

Wakati waimbaji hao wengine bado hawajaanza kuhusishwa na uhamisho wa kwenda bendi nyingine, Mishi ana anahusishwa sana na Yah TMK.

Saluti5 ilipomuuliza Mishi juu ya uvumi huo wa kujiunga na Yah TMK, hakukanusha waka kukubali.

Mishi alisema: “Mimi nina madai yangu Jahazi ambayo kwasasa sina haja ya kuyaweka wazi. Yah TMK ni bendi kubwa na inanivutia kufanya nayo kazi.

“Kama nitaondoka Jahazi basi sitakuwa msanii wa kwanza kufanya hivyo wala sitakuwa wa mwisho. Jahazi ni bendi yangu na ninaipenda lakini maisha popote. Baada ya wiki mbili nitaweka wazi hatma yangu”.

Kuhusu kuonekana kwenye jukaa la Yah TMK, Mishi alisema bendi ile ni kama nyumbani kwake kwa vile ina wasanii wengi aliofanya nao kazi Jahazi.

Uongozi wa Jahazi umeiambia Saluti5 kuwa wasanii hao watano wametakiwa kuandika barua ya kuomba radhi kabla ya kurejeshwa kazini, lakini habari za ndani kabisa zinadai kuwa kuna wasanii ambao hawako tayari kuomba radhi huku wengine wakiwa mbioni kuandika barua ya kukiri makosa.No comments