MOHAMMED MKOPI WA MBEYA CITY ATAMBA KUIMALIZA MBAO FC

MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa na Mbeya City, Mohamed Mkopi amesema kwamba wana uhakika wa kuondoka na alama zote tatu katika mchezo wao ujao dhidi ya timu ya Mbao FC kwenye uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Mkopi amesema kuwa kocha waliompata hivi sasa, Ramandan Nsanzurimo Ramadhani amekuwa akiwapa hamasa ya ushindi katika mechi za ugenini sambamba na program za mazoezi ambazo zinafurahiwa na kila mchezaji kikosini hapo.

Mkopi amecheza jumla ya dakika 365 mpaka sasa na katika mchezo uliopita aliweka wavuni goli lake la kwanza dakika ya 78 ya mchezo wa sare ya mabao 2-2 dhidi ya timu ya Mwadui.

“Msimu iliopita haukuwa mzuri sana kwangu kwasababu kichwa kilitawaliwa na mawazo baada ya kuwa na adhabu na kutojihusisha na Ligi kwa msimu mzima kufuatia adhabu niliyopewa lakini sasa nina sababu ya kucheza kwa kiwango  cha juu na hata mechi yetu ijayo naamini tutafanya vizuri,” alisema mshambuliaji huyo.

“Tumebahatika kupata kocha anayeeleweka lakini pia amekuwa mtu wa kutupa hamasa ya kushinda kila wakati, yeye ni ushindi tu,” aliongeza.

Kocha Ramadhani ameanza kukiokoa kikosi hicho kilichokuwa chini ya mwalimu Mohammed Kijuso toka kuanza kwa Ligi Kuu msimu huu baada ya kushindwa na Kinnah Phiri. Mbeya City inakamata nafasi ya saba huku Mbao FC wanakamata nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara.


Mchezo huo hautarajiwi kuwa rahisi kutokana na tabia ya Mbao kuwa wagumu katika mechi wanazochezea kwenye uwanja wanyumbani kwani hata Simba waliambulia sare ya mabao 2-2 bila kutarajia.

No comments