MOURINHO NDO ZAKE, MISIMU MIWILI AU MITATU ANAKUACHIA TIMU LAKO …Man United yaanza kuishi kwa mashaka


Jose Mourinho amesema utakuwa ni mpango usiowezekana kwa yeye kufikiria kuwa atamalizia kazi yake ya ukocha Manchester United.

Wikiendi iliyopita Mourinho aliirusha roho Manchester United baada ya kunukuliwa akionyesha kuvutiwa na Paris Saint-Germain, hali iliyowafanya wachambuzi wa soka waamini kuwa kocha huyo anaanza kujiandaa na safari ya kutimka Old Trafford.

Akiongea Jumanne mchana kuelekea mchezo wa Champions League dhidi ya Benfica, Mourinho akasisitiza kuwa hana mpango wa kuondoka Old Trafford - lakini bado hajaingia kwenye mazungumzo ya mkataba mpya.

"Mkataba wangu unaisha mwaka 2019, sasa ndiyo kwanza tupo Oktoba 2017, sielewi haya mambo mengine yanatokea wapi," alisema Mourinho.

Kocha huyo akaongeza: "Hivi karibuni mlisema ninasaini mkataba mpya wa miaka mitano, sasa mnakuja na hadithi ya mimi kuondoka Manchester United.

"Kitu pekee mlichoninukuu kwa usahihi ni juu ya kali yangu kuwa sitastaafu kazi nikiwa Manchester United, hili nilitamka na huo ndiyo ukweli, lakini haimaanishi kuwa naondoka hivi karibuni.

"Kwa utamaduni wa soka la sasa hivi, hakuna tena klabu itakayodumu na kocha mmoja kwa miaka mingi. Namuona Arsene Wenger akiwa kocha wa mwisho kuhitimisha utamaduni huo wa kukaa muda mrefu kwenye klabu moja".

Tangu Mourinho aanze kufundisha timu kama kocha mkuu mwaka 2000 kupitia Benfica na baadae Porto, Chelsea, Inter Milan, Real Madrid hadi kurejea Chelsea mwaka mwaka 2013 hadi 2015, hajawahi kuikochi timu moja kwa zaidi ya misimu mitatu mfululizo.

No comments