MUUMIN ASEMA ASHA BARAKA ALIIPENDELEA TWANGA PEPETA KULIKO TAM TAM


Aliyekuwa kiongozi wa The African Revolution “Tam Tam” Mwinjuma Muumin amesema mmiliki wa bendi hiyo Asha Baraka aliipendelea zaidi Twanga Pepeta.

Akiongea na kituo cha 98.5 AM FM Radio, Muumin akasema Asha Baraka ukimchanja, basi damu yake ni Twanga Pepeta.

Twanga Pepeta na Tam Tam zote zilimilikiwa na Asha Baraka ambapo Tam Tam ilitingisha sana mwanzoni wa miaka ya 2000 kabla kufa kifo cha kawaida miaka michache baadae.

“Tam Tam ilikuwa juu sana na ingawa tulikuwa hatutafutiwi mavazi mazuri kama Twanga Pepeta, lakini bado tuliteka mashabiki, sisi hata tulipokuwa tunavaa magwanda ya kuokotaokota, bado tulikuwa hatari jukwaani,” alieleza Muumin.

“Swahima wangu, mama yangu Asha Baraka alikuwa hatujali sana kwa mavazi, yeye aliiangalia zaidi Twanga Pepeta. Hata tulipokuwa tukifanya show ya pamoja, alikuwa mkali pale inapotokea gazeti fulani likaandika Tam Tam yaifunika Twanga Pepeta,” alifichua Muumin.

No comments