MUUMIN: BUBU PEKEE NDIYE HAWEZI KUIMBA


Mwinjuma Muumin “Kocha wa Dunia” amesema yupo tayari kumfundisha mtu yeyote kuimba kwa vile anaamini kila mtu ana uwezo wa kuimba ili mradi tu awe anaupenda muziki.

Muumin amesema anapenda kuona damu mpya ya waimbaji kwenye muziki wa dansi na ndiyo maana mara nyingi amekuwa akiibuwa waimbaji wapya.

“Kwasasa ninaye mwimbaji wa kike Salma Mjukuu, huyu nimemtoa kwenye unenguaji hadi uimbaji, anafukia mashimo yote ya nyimbo zilizoimbwa na Hadija Kimobitel na marehemu Amina Ngaluma na wengineo,” anaeleza Muumin, mmiliki wa Double M Sound.

“Kama kuna mtu anahisi ana kipaji cha kuimba basi aje nitamfundisha bila gharama yoyote, mimi naamini asiyejua kuimba ni bubu tu, lakini mtu mwingine yeyote anaweza kuimba,” alifafanua Muumin katika maongezi yake na kipindi cha Michapo cha 98.5 AM FM Radio.
No comments