RYAN GIGGS ASEMA MOURINHO AMESHAMPATA MBADALA WA PAUL POGBA

Gwiji wa Manchester United Ryan Giggs amesema tayari Jose Mourinho ameshampata mtu wa kuziba pengo la Paul Pogba aliye majeruhi.

Kiungo huyo wa pauni milioni 89 yuko nje ya dimba kwa maumivu ya msuli, lakini Manchester United imeendelea kufanya vizuri bila uwepo wake.

Mourinho amekiri kuwa Pogba bado atakuwa nje uwanja kwa muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa.

Lakini Giggs anasema Marouane Fellaini amekuwa mtu muhimu katika mafanikio ya Manchester United bila Pogba.

"Marouane Fellaini amethibitisha umuhimu wake, akiziba vema pengo la Paul Pogba," anaeleza Giggs katika maongezi yake na Sky Sports. "Amefunga magoli muhimu kama alivyokuwa akifanya Everton.

"Nimewahi kufanya naye kazi, ni mtu bora kabisa kwa kuwa anafanya kile unachomwelekeza na hakubali kuyumbishwa na kebehi za mashabiki kwa kuwa anaungwa mkono na wachezaji wenzake na makocha."

Giggs akaongeza: "Yuko vizuri, anajua uwezo wake na majukumu yake. Mourinho amemwamini na yeye anamlipa kwa kufunga magoli muhimu."

No comments