AYA 15 ZA SAID MDOE: SALUTI KWENU TANZANIA BAND FESTIVAL, MAZURI YALIKUWA MENGI KULIKO MAPUNGUFU


TAMASHA la bendi za Tanzania (Tanzania Band Festival) lililofanyika mjini Dodoma usiku wa kuamkia leo, haliwezi kupita hivi hivi bila kusema chochote.

Onyesho hili limefanyika ndani ya Kisasa Capetown Complex na kuhudhuriwa na watu wa kutosha huku bendi tano – Malaika Band, B Band, Twanga Pepeta, Msondo Ngoma na FM Academia zikichuana jukwaani.

Jambo jema zaidi ni kwamba tofauti na mwaka jana ambapo show ilifanyika moja tu jijini Dar es Salaam, safari hii Tanzania Band Festival imetanuka zaidi na kwenda hadi mikoani.

Kabla ya onyesho hili la Dodoma, Tanzania Band Festival ilifanyika katika miji ya Kahama na Mwanza. Nimeambia kuna mikoa mingi ipo kwenye foleni ya tamasha la mwaka huu. Hili ni jambo la kupongezwa na kwa hakika linastahili kuungwa mkono.

Kama nilivyowahi kusema mwaka jana, tamasha hili linapaswa kuwaamsha wadhamini ambao wamekuwa wakiwekeza nguvu nyingi kwenye muziki wa kizazi kipya ambao hutawaliwa zaidi na mfumo wa kutumia CD (Playback). Nashukuru kwamba mwaka huu wadhamini wengi wameanza kujitokeza.

Nikasema muziki wa bendi (live) hususan ule wa dansi, ndiyo muziki wa ukweli, muziki ghali, muziki unaotoa ajira kubwa, hivyo anapotokea mwandaaji kama Q Plus, umma wa wapenda dansi unastahili kushukuru na kuunga mkono hasa kutokana na ukweli kuwa ‘wawekezaji’  (mapromota) wengi hawaamini katika kuwekeza kwenye muziki wa dansi. Nafurahi kuwa wadau wamezidi kulielewa tamasha hili.

Lakini pamoja na mema yote ya onyesho hili la Dodoma, bado kuna dosari ndogo ndogo za hapa na pale ambazo zinastahili kurekebishwa na kwa bahati mbaya dosari nyingi kati ya hizo ni zile zile nilizozitaja mwaka jana, sijui kama zinafanyika kwa bahati mbaya, makusudi au kwa upungufu wa uelewa wa mambo kwa watu waliokabidhiwa majukumu fulani fulani ya tamasha hilo.
Muda wa kuanza kwa onyesho: Mwaka jana ilitangazwa kuwa kuwa onyesho lingeanza saa 5 asubuhi lakini likaanza saa 12 jioni. Dodoma matangazo yote yakasema show itaanza saa 10 jioni lakini ikaanza saa 4 usiku. Haya ni makosa ya kiufundi ambayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kuathiri mahudhurio ya onyesho.

Muda wa bendi kukaa jukwaani: mwaka jana tuliambiwa kila bendi itakaa jukwaani kwa dakika 45, lakini baadae zikapungua hadi 30 na mwishowe ikawa 20 – hii maana yake ni kwamba waandaji hawakupiga hesabu nzuri za masaa ya onyesho lao kwa kugawanya na idadi ya bendi. Mwaka huu hili limejirudia tena.

Wakati Msondo Ngoma waliofungua pazia la show walitumbuiza kwa dakika 50 tu huku wakipiga nyimbo nne, B Band waliofutia wakatumbuiza mara mbili ya muda waliotumia Msondo na kutandika zaidi ya nyimbo kumi. 

Kituko kingine kikawadia, wakati B Band wameshuka na MC akapoteza zaidi ya robo saa kwa gumzo lisilo na lazima kabla hajatuambia Twanga Pepeta wanapanda jukwaani, mara MC huyo akarejea na hoja kuwa kuna shabiki muhimu ameomba B Band wapande tena kupiga wimbo mmoja na kweli ikawa hivyo. Yakaibuka manung’uniko mengi kwa mashabiki. Haya yalikuwa makosa makubwa ya upotezaji muda.

FMAcademia iliyofuata baada ya B Band, ikatumbuiza kwa muda usiozidi dakika 50 wakapiga sebene moja na nyimbo mbili “Wanawake” na Dunia Kigeugeu”. Bendi zilizofuatia – Malaika na Twanga nao walitumbuiza kwa muda usiozidi dakika 60, onyesho likaisha saa 10 usiku kitu ambacho kinamanisha kuwa onyesho lingemalizika saa 9 usiku iwapo B Band wangekaa jukwaani kwa muda wa dakika 50. Bado sioni hekima iliyotumiwa na MC kuiacha B Band jukwaani kwa takriban saa mbili.

Dhumuni la tamasha: Tangu mwaka jana hadi leo hii, wengi tulidhani ni tamasha la muziki wa dansi na kwa hakika hivyo ndivyo tulivyoaminishwa, lakini inaelekea waandaaji hawalisimamii hilo ipasavyo.

Mwaka jana tulishudhia tamasha  likipambwa pia na muziki wa reggae, chakacha,pop n.k, na ndivyo pia ilivyokuwa kwenye onyesho la Dodoma ambapo B Band ilipiga nyimbo nyingi za kizungu ambazo hakikuwa na mahadhi ya dansi wala rumba. Ipo haja ya waandaji kuzipatia sara ya tamasha bendi shiriki. Sielewi pia ni kwanini bendi za Dodoma hazijashirikishwa.

Yote kwa yote yote niseme onyesho lilikuwa zuri, mambo mema, mazuri na yenye tija yalikuwa mengi kuliko mapugufu yaliyojitoeza. Hongereni sana O Plus Entertainment, hongera kwa bendi shiriki. Bendi iliyonivutia sana ni FM Academia, mwimbaji aliyenikosha sana ni Christian Bella, mpiga ala aliyenimaliza zaidi ni Fred Manzaka wa FM Academia. Wasanii walionikera ni Kaposhoo, Miraji Shakashia na Hajj BSS ambao walirudia sare zao walizozitumia kwenye tamasha la mwaka jana.No comments