YANGA, SIMBA NI VITA YA KUFA MTU LEO UWANJA WA UHURU DAR

MECHI ya Yanga na Simba inayopigwa baadae leo kwenye dimba la Uhuru, jijini Dar es Salaam inazalisha mechi nyingine ndani yake kati ya kocha George Lwandamina raia wa Zambia na Mcameroon Joseph Omog.

Makocha hao watatakiwa kuthibitisha ubora wa mbinu zao na kuhakikisha wanaleta ushindi kwa timu wanazofundisha lakini pia kuandika rekodi ya nani amemfunga mwenzie mara nyingi zaidi katika mechi za watani wa jadi.

Makocha hawa watakutana kwa mara ya nne ambapo kabla ya hapo walishakutana kwenye michezo mitatu ya mashindano yote ya VPL, Mapinduzi Cup na Ngao ya Jamii ambapo katika mechi zote hizo kocha Joseph Omog amefanikiwa kushinda mechi mbili kwa njia ya penati na moja alishinda katika dakika tisini za mwamuzi.

Kufuatia hali hiyo, kocha wa timu ya Yanga, George Lwandamina amesema kuwa haumizwi na masuala ya rekodi na anachojali ni kushinda katika mchezo huo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kukaa kileleni mwa Ligi.

Nae Omog amesema kuwa timu yake iko vizuri kukabiliana na yoyote na hata mazingira tulivu ya kambi waliyoweka yamezidi kuongeza hali ya ushindi huku akisema kuwa ni mchezo ambao watacheza kufa na kupona kwasababu ushindi kwao utawafanya kuendelea kung’ang’ania kileleni.

Kwa mara ya kwanza, Omog na Lwandamina walikutana Januari 10, 2017 katika mchezo wa nusu fainali ya Mapinduzi Cup visiwani Zanzibar. Simba walishinda kwa penati 4-2 baada ya kutoka suluhu ya 0-0 ndani ya dakika 90.


Timu hizo zinaingia uwanjani zikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda katika mechi zao za mzunguuko wa sita wa Ligi Kuu Tanzania bara ambapo zote zilitoa kipigo cha mabao 4-0.

No comments