YANGA, SIMBA PRESHA JUU KUELEKEA PAMBANO LA OKTOBA 28

JOTO la mechi ya watani wa jadi Oktoba 28, limeanza kupanda ambapo klabu ya Simba imepanga kuweka kambi yake visiwani Zanzibar kama kawaida yao huku kocha wa Yanga, George Lwandamina akisema kuwa hana mashaka na kikosi chake.

Ligi Kuu wikiendi iliyomalizika jana ilikuwa kwenye mzunguko wake wa saba lakini klabu za Simba na Yanga macho yote yapo Oktoba 28 ambapo timu hizo zitakutana kwa mara ya kwanza katika mechi za Ligi msimu huu.

Kocha wa timu ya Yanga Lwandamina amesema kuwa anajivunia ubora wa safu yake ya ushambuliaji ambayo imeonekana kuanza kuimarika ikiongozwa na mshambuliaji Ibrahim Ajib huku upande wa Simba wao tayari wameshabomoa benchi lao la ufundi baada ya kutemana na kocha msaidizi, Jackson Mayanja.

“Najua utakuwa mchezo wa presha kubwa lakini kikosi changu kipo tayari kwa mechi hiyo, mwanzoni kulikuwa na mapungufu kwenye safu ya ushambuliaji lakini sasa naona kuna uwelewano mzuri umeanza kujengeka na kunipa imani ya kufanya vyema,” alisema kocha huyo.

“Tuna kikosi kipana sasa na majeruhi wanazidi kupona hivyo sioni haja ya kuwa na hofu kwa mashabiki kwasababu tumejipanga kuwafurahisha,” aliongeza.


Simba na Yanga zinakutana huku zikiwa na kumbukumbu ya mchezo wa ngao ya hisani ambapo Simba waliibuka na ushindi kwa njia ya mikwaju ya matuta baada ya dakika tisini kuisha kwa sare.

No comments