YANGA YAPANGA KUMPIGIA MAGOTI MANJI AREJEE JANGWANI

YANGA haitaki kupoteza muda na akili ya wengi sasa ni kutaka kuona mwenyekiti wao, Yusuf Manji anarudi katika nafasi yake, lakini usichofahamu ni kwamba katibu mkuu wa timu hiyo, Charles Mkwasa ametamka kwamba wanamfuata bilionea huyo.

Mkwasa ameyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba klabu yao imefarijika kwa kuachiwa huru kwa Manji akishindwa kuwekwa hatiani kwa kesi ya matumizi ya dawa za kulevya.

Katibu huyo amesema hatua ambayo ipo kwao kwa sasa ni kujipanga kumfuata Manji kwanza, kumpa pole kwa matatizo yaliyokuwa yakimkabili lakini pia watamfikishia salamu za Wanayanga ambao kwanza walishindwa kukubali maamuzi yake ya kujiudhuru majukumu hayo na zaidi wakitaka sasa arudi.

“Unajua hizi ni taarifa njema kwetu kwa Manji kuwa huru, hii hata mimi binafsi inanifariji kwa kuwa mimi ndiye niliyemuwekea dhamana katika kesi hii na anapokuwa hana kesi ya kujibu hata mimi inanipa uhuru,” alisema Mkwasa.

“Unajua Yanga bado nafasi ya Manji ipo, sasa ametoka kama uongozi tunajipanga kumfuata na kuongea naye kwa kumpa pole lakini pia salamu za Wanayanga ambao walikataa kukubali maamuzi yake ya kujiuzulu na zaidi wanataka kumuona sasa anarudi na kiukweli nafasi yake bado ipo.”

Wakati Mkwasa akiyasema hayo juzi Jumamosi, viongozi wa matawi wa Yanga walikutana makao makuu ya klabu hiyo ambao walikazia maamuzi yao ya kutaka Manji arudishwe wakimtaka Makamu mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga kufanya hivyo.

Nyuma ya hilo Manji mwenyewe inaelezwa kwamba hana kinyongo katika kurudi katika klabu hiyo kutokana na kwamba aliamua kujiuzulu akihofia kuchafua jina la klabu hiyo katika kesi hiyo ya dawa za kulevya iliyokuwa ikimkabili ambapo sasa kuwa kwake huru kunamfanya kuvuta kasi ya kurudi.

No comments