AYA 15 ZA SAID MDOE: DANSI NA HADITHI YA MUUGUZAJI ANAFARIKI, MGONJWA ANAJIKONGOJA


Niliwahi kusema kuwa tatizo kubwa linaloikabili ‘kiwanda’ cha muziki dansi, ni ile hali ya  kizazi bora cha wanamuziki bora wa dansi kupungua mwaka hadi mwaka. Hakuna uwiano mzuri wa wanaochuja na wanaoibuliwa.

Sidhani kama baada ya mwaka 2007, kuna mwimbaji mpya wa dansi ameibuka mwenye uwezo wa Banza, Chocky, Rogart, Muumin, Bella, Jose Mara, Chokoraa, Chaz Baba, Kalala Jr, Pablo Masai, Mule Mule, Tarsis Masela, Badi Bakule na wengine wengi wa ubora huo. Kizazi hiki kinahitaji kupokewa, lakini wakowapi wa kuwapokea? Kama wapo je ni kweli wanafikia hata nusu ya uwezo wao?

Hili ni janga kwa muziki wa dansi na ndio linapelekea kukosekana kwa ‘hit song’, hakuna mwimbaji mpya wa dansi aliyeibuka baada ya mwaka 2007 halafu akafanikiwa kuweka muhuri wake kwenye wimbo wowote.

Muhuri ninaouzungumzia ni kama walivyoweka wenzao alama zao kwenye nyimbo kama “Tunda”, “Mtu Pesa” “Dunia Kigeugeu” “Jirani”, “Mgumba”, “Double Double”, “Yako Wapi Mapenzi” na nyingine nyingi. Hizi ni aina ya nyimbo ambazo kila kipande cha mwimbaji kilipata umaarufu na kukubalika.

Wachache walioonekana kuwa warithi wapya wa muziki wa dansi, walipotea hata kabla majina yao hayakaa vilivyo kwenye ramani ya muziki wa dansi. Ziko wapi kazi za vijana kama Athanas Montanabe, Anko Venna, January Eleven, Jimmy Gola, Dogo Hija (Muumin Junior) na wengineo wa rika hilo? 


Kipindi fulani katika bendi ya Mapacha Watatu kulikuwa na kijana anaitwa Kambi, alikuwa mwimbaji anayeinukia vizuri, lakini katika umri wake mdogo akaamua kujichakaza na pombe, akazimika kisanii kabla hajafika popote na hadi leo hii sijui yuko wapi na anafanya nini.

Kuna bwana mdogo mmoja anakwenda kwa jina la Melody Mbasa, huyu aliibua matumani kwa wapenzi wa dansi, akaachia kigongo kikali kilichoitwa “Nikukoleze”.

Kijana anajua kuimba, ana melody tamu, akafanya kila kinachohitajika kwenye soko la sasa la dansi, akausindikiza wimbo wake na video kali. Nikasema ‘naam, namuona Christian Bella mpya kwenye muziki wa dansi’. Lakini takriban mwaka mzima sasa tangu wimbo huo uingine hewani, kijana huyu ameshindwa kuachia kazi nyingine mpya na kali itakayotuthibitshia ubora wake.

Kwa soko la sasa, si sahihi kwa msanii au bendi kumaliza miezi minne bila kazi mpya, dunia inakwenda mbio sana, vijana wa bongo fleva wanafyatua nyimbo mpya kama hawana akili nzuri. Wanafanya hivyo kwa vile wanajua mauzo ya show zao yanatokana na nyimbo mpya.

Msanii chipukizi kama Melody Mbassa anabahatika kuachia nyimbo halafu ikakubalika na kisha kuichezea nafasi hiyo kwa kukaa mwaka mzima bila kutoa nyimbo mpya, ni sawa na kuchezea pesa kwenye tundu la choo.

Katika kipindi cha Buzuki cha Capital Radio kinachoruka jioni kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa, nimekuwa nikikutana na ‘jingle’ ya Melody Mbassa ya kunadi kipindi hicho, lakini ndani yake nikapatwa na mshangao mkubwa na kujiuliza iwapo kijana huyu anataka kuwa yeye kama yeye au anataka kuwa ‘photocopy’ ya wasanii nyota.

Ndani ya tangazo hilo fupi la kunadi kipindi cha Buzuki, Melody Mbassa anasikika akiimba vipande nyimbo za Fally Ipupa na Ferre Gola, halafu anataja jina lake kwa mbwembwe nyingi kupitia lafudhi ya Kicongo.

Najiuliza ni kwanini Melody Mbassa hakutaka kupromoti wimbo wake wa “Nikukoleze” katika jingle hiyo ya kipindi cha Buzuki? Kipi chenye faida na yeye kati ya “Nikukoleze” na nyimbo za kina Ferre Gola?. Kwanini basi hata asitumie nafasi hiyo kuchomekea vipande vya kazi zake mpya zijazo? Naamini hii ni dalili ya kutojitambua.

Vijana wa kizazi kijacho cha dansi inabidi wajitambue, wajue kusoma alama za nyakati na wajifunze kupitia makosa na mazuri ya waliowatangulia. Kinyume na hapo hawatatofautina na ile hali muuguzaji anafariki huku mgonjwa akiendelea kujikongoja.


No comments