AYA 15 ZA SAID MDOE: LINI ATATOKEA MTU WA KUSULUHISHA ‘UGOMVI’ WA DANSI NA FIESTA?


Tamasha la Tigo Fiesta 2017 lilifikia kilele chake Jumamosi usiku kwenye viwanja wa Leaders Club jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu.

Hakuna ubishi kuwa ‘fainali’ ya Fiesta ambayo hufanyika Dar es Salaam, ndiyo tukio kubwa zaidi la kimuziki kuliko lolote lile Tanzania kwa maana ya mahudhurio, ukubwa wa majina ya  wasanii wanaokwea jukwaani, ubora wa maandalizi, fitna za promosheni na usalama wa watu na mali zao.

Nilikuwepo Leaders Club Jumamosi kujionea namna tamasha hilo la kipekee lilivyobamba. Hakika tamasha hili limenifanya niiheshimu sana Clouds Media Group, hii ‘taasisi’ iko mbali sana katika masuala ya burudani, simuoni kiumbe mwingine au taasisi nyingine inayoweza kuukusanya umati kama ule kwa kiingilio kisichopungua shilingi 10,000 na kuuweka pale hadi afajiri.

Ziko taasisi nyingi sana ambazo zimeshawahi kuandaa matukio makubwa ya burudani yenye utitiri wa wasanii wakubwa wenye majina yao, wa ndani na nje ya nchi, lakini mahudhurio wanayoyaokota huwa ni kituko, hasara tupu.

Jambo jema ni kwamba kwa mwaka wa pili mfululizo, karibu asilimia 90 ya wasanii waliotumbuiza kwenye Fiesta, walitumbuiza kwa kupigiwa vyombo (live), taratibu Fiesta inaanza kuachana na muziki wa maigizo (playback).

Kwenye live ndiyo   patamu sana, mfumo huu unatusaidia kuwajua wasanii wa ukweli na wasanii wa kuchovya, wako mastaa wengi walitia aibu Jumamosi kwa kuonyesha kiwango duni cha kutumbuiza kwa mfumo wa 'live band'.

Nilishuhudia msanii mmoja mkubwa sana, aliyetegemewa na wengi kuiteka show, akitumbuiza katika kiwango cha kawaida sana, akafunikwa na wasanii wengi sana na hata baadae nilipo bahatika kutupia macho kipande cha video alichokitupia Instagram, nikacheka sana, ilijaa ‘uhariri’ usioendana na hali halisi.

Mkali huyo aliweka video ya matukio ya Leaders lakini akaminya sauti (mute) ya Leaders  na badala yake akaweka sauti ya kutoka kwenye CD ya wimbo wake maarufu …picha ya Leaders lakini  sauti ya studio. Hii ni dalili tosha kuwa hata yeye binafsi hakuridhika na kile alichokifanya Leaders.


Na hapo ndipo ninapouona umuhimu wa wanamuziki wa dansi katika maonyesho makubwa kama ya Fiesta, wasanii wa dansi sio wa kubezwa, wana nafasi kubwa ya kuwafunza wasanii wa kizazi kipya miiko, njia na mbinu za uimbaji muziki wa ‘live’.

Kama Fiesta sasa inakwenda kwa mfumo wa wasanii kusindikizwa na ‘live band’, sioni ni kwanini isirudishe utaratibu wake wa zamani wa kuwatumia wasanii nyota wa dansi. Sielewi ni nini kilitokea hadi Clouds Media Group wakawafungia milango wasanii wa dansi kwenye Fiesta. Jamii kubwa ya wanamuziki na mashabiki wa dansi inalia na Clouds Media kuwa ‘imeuminya’ muziki wa dansi si katika matamasha yao tu, bali hata kwenye vituo vyao vya radio na televisheni.

Fiesta imekuwa ni tamasha la wasanii wa kizazi kipya. Mwimbaji pekee wa dansi aliyetumbuiza kwenye Fiesta ni Christian Bella, msanii mwingine kutoka nje ya bongo fleva aliyefanya vitu vyake Leaders Club ni Isha Mashauzi. Kwa mshabiki mwenye kuujua muziki na mwenye sikio zuri la muziki ni wazi kuwa atakuwa amegundua ubora wa uimbaji wa Bella na Isha kulinganisha na wasanii wengi wa kizazi kipya.

Sielewi ni ugomvi gani au hila gani iliyoingia baina ya Fiesta na wasanii wa dansi. Najua bendi nyingi za dansi ni sugu katika kurefusha nyimbo bila sababu za msingi, ni sugu wa hila za kutaka kurekebisha vyombo (ku-tune) hata pale pasipo hitajika kufanya hivyo.

Najua pia kuwa bendi nyingi ni sugu katika kutupia mavazi yasiyo na mvuto wa kisanii, sugu kwa kuvaa mavazi ya kizamani, sugu kwa mavazi ya kutupia tupia na ya bei ya chini, lakini haya yote yanaweza yakarekebishwa kutegemea na masharti na utashi wa mwenye tamasha lake.

Katika matamasha ya Kili Music Awards ambayo naamini kwa namna mmoja au nyingine,  mkono  wa Clouds Media ulihusika kuratibu,  tuliwahi kushuhudia wasanii wa dansi na taarab kama Hussein Jumbe, Chaz Baba, Jose Mara, Khalid Chokoraa, Mzee Yussuf na Patricia Hillary  wakiimba nyimbo maarufu za dansi na taarab kwa kwa mfumo wa kisasa kwa kushirikiana na nyota wa kizazi kipya kama Barnada, Amin na Linah na kutoa matokeo chanya ambayo yalikuwa kivutio cha kipekee. Kwanini Clouds hawafanyi hivyo katika Fiesta?

Si lazima warundike bendi kibao katika Fiesta, lakini wanaweza wakachagua bendi tatu halafu wakatengeneza mfumo utakaowezesha bendi hizo kupigiwa na wapiga vyombo wale wale, mazoezi ya wiki moja tu yanatosha kuwezesha zoezi hilo. Kati ya hizo bendi tatu kila moja ikipiga nyimbo moja au mbili za muda usiozidi dakika 10, basi naamini Fiesta itakuwa chachu ya kuurudisha muziki wa dansi kwenye chati. Chonde chonde Clouds Media fanyeni juhudi za makusudi za kuunyanyua upya muziki wa dansi.


No comments