AYA 15 ZA SAID MDOE: SHAIBU MAPAJERO, FIKIRI MADINDA, DR RAMA, AKIDA TRANS, KIZAIZAI SUPER TALL!!


Leo nimejisikia tu kukumbuka wadau wa muziki wa dansi ambao kwa namna moja au nyingine walichangia kuupandisha muziki wa huu huku pia muziki wa dansi ukichangia kupandisha majina yao.

Wako wengi sana na wala sina hata haja ya kutaja majina yao, niliowataja kwenye kichwa cha habari wanatosha kuwa wawakilishi wa utitiri wa watu ambao waligeuza kabisa utamaduni wa muziki wa dansi kuanzia miaka ya mwishoni mwa tisini.

Naam nasema walibadili utamaduni wa muziki wa dansi kwa kuwa huko nyuma jina la binadaamu yeyote linalotajwa (fagio) kwenye wimbo, basi ilikuwa ni lazima liwe la mwanamuziki, aidha mwimbaji anakaribishwa kwenye kipande chake atakachoimba au mpiga ala, si zaidi ya hapo.

Pengine pia utaratibu huu usingekuja kama si ujio wa watu walioitwa ma-rapa kwenye muziki wa dansi, hawa ndio watu waliotuletea hili balaa lote la kutujazia majina ya watu kwenye nyimbo kiasi kwamba inafika wakati hata wimbo wenyewe hauleweki.

Lakini pia yote hii imekuja kutokana na ‘ubwege’ wetu wa kuiga au kuhamisha kila jambo jipya linaloingia kwenye muziki wa Kikongo, yaani wale wamekuwa ndiyo manahodha wetu – wanatupeleka wanavyotaka.

Kuanzia mwaka 1996 au 97 kama sikosei, bendi ya Diamond Sound “Ikibinda Nkoi” ilitubadilishia kabisa mwelekeo wa muziki wa dansi na hapo ndipo tulipoanza kusikia utitiri wa majina ya wadau na mapedeshee kwenye nyimbo kupitia kinywa cha rapa Alain Mulumba Kashama ambaye kwa wakati huo alikuwa staa zaidi ya ujuavyo. Jamaa aliandika historia, tuache masihara!


Baada ya hapo, bendi zote zilizochanua mgongoni mwa Diamond Sound, zikafuata mkumbo, si FM Musica (FM Academia), si Twanga Pepeta wala Achigo Band, ili mradi kila bendi iliamini katika kutandika masebene na kujaza majina ya wadau mwanzo hadi mwisho wa wimbo.

Wakati mwingine ujumbe wa maana wala haukuwa dili katika baadhi ya nyimbo zao – majina na vionjo vya rap vilitosha kukamilisha.

Wadau hawa waligawanyika katika makundi mengi: wako waliotajwa kwa ajili ya umuhimu wao kwenye tasnia ya muziki wa dansi, wako waliotajwa kutokana na urafiki baina yao na wanamuziki, lakini wako pia waliotajwa kutokana na juhudi zao za kuwafadhili wanamuziki na bendi kwa ujumla na hawa ndiyo nitakaopendelea zaidi kuwazungumzia leo hii.

Wadau hawa wanaotajwa kwa ufadhili wao, walikuwa na nguvu kubwa sana ya kulisongesha gurudumu la muziki wa dansi, lakini nguvu yao ilikuwa ni ya muda mfupi na wengi wao hawakuwa mashabiki wa kweli wa dansi, bali waliingia kwa malengo maalum.

Wako walioingia kwa malengo ya kisiasa, wako walioingia kwa ajili ya kutangaza biashara zao kwa njia ya mkato, wako walioingia ili kukuza majina yao. Kipindi hicho muziki wa dansi ulikuwa juu sana na hivyo ilikuwa rahisi kwao kukamilisha malengo yao kupitia muziki wa dansi, wakisharidhika na mavuno yao wanatokomea kusikojulikana.

Na ndio maana wengi wao kati ya utitiri wa majina yaliyowika sana enzi hizo, leo hii huwasikii tena, huwaoni kwenye kumbi za dansi wala huwaoni katika harakati za kuukwamua muziki wa dansi. Sababu kuu za kutoonekana kwao ziko tatu.

Sababu ya kwanza ni kwamba muziki wa dansi umeshuka na hivyo hawahitaji kupoteza nguvu zao kwa kitu ambacho hakitawapa uwanja mpana wa kujitangaza. Sababu ya pili: Wako walioporomoka kiuchumi na hivyo hawana tena jeuri ya kuusogelea muziki wa dansi mikono mitupu – hawajazoeleka hivyo. Sababu ya tatu: Wako ambao waliingia kwa malengo maalum ya kutangaza majina yao ili kupata urahisi wa kupenya sehemu fulani fulani, malengo yao yametimia hivyo hawauhitaji tena muziki wa dansi.

Hawa watu walitumia nguvu kubwa sana kuupandisha muziki wa dansi (japo ni kwa malengo yao maalum), baadhi yao walikuwa wanakwenda studio kila bendi inaporekodi na kuhakikisha wanamuzuki na producer  wanakula vizuri katika muda wote wanaokuwepo studio, ikibidi na nauli pia ilikuwa juu yao.

Walikuwa wana nguvu kubwa ya kuusukuma wimbo kwenye vituo vya radio maana hata baadhi ya watangazaji pia waliwekwa chini ya himaya yao. Walitatua shida nyingi za bendi ikiwemo sare na kodi za nyumba za wanamuziki, kufadhili kambi za uzinduzi wa albamu mpya, kugharamia usajili wa wanamuziki wapya katika bendi n.k.

Natamani sana watu hawa wangedumu kwenye muziki wa dansi, natamani uwepo wao ungekuwa ni kwa ajili ya mapenzi ya dhati kwa muziki wa dansi. Nathubutu kujiridhisha kuwa upepo huu wa kuyumba kwa soko la dansi ungekuwa wa muda mfupi sana, naamini wadau hawa wangeupigania kwa nguvu kubwa za kiuchumi na kuurudisha kwenye reli muziki wa dansi.

No comments