AYA 15 ZA SAID MDOE: WEWE NI SAWA NA KIAZI KWENYE PILAU


Unaambiwa ubora wa pilau ni pamoja na uwepo wa nyama za kutosha, ila kiazi ni kitu cha ziada tu, kiwepo kisiwepo bado thamani ya pilau iko pale pale.

Lakini hata katika maisha yetu wako watu ambao nafasi zao katika taasisi zao ni kama kiazi kwenye pilau, wanachukuliwa kama watu wa kawaida sana aidha kwa hali halisi ya uwezo wao au kwa namna wanavyojiweka, watoto wa wa mjini wanasema ‘kujibrand’.

Wewe ni msanii wa bendi, iwe ya dansi au taarab au kundi lolote la muziki? Umeshawahi kuupima umuhimu wako kwenye kundi lako? Umeshawahi kuitathmini thamani yako?

Umewahi kujiuliza hata siku moja iwapo wewe ni kiazi au nyama kwenye pilau? Unajua kuwa kwenye bendi zetu kuna viazi vingi na pengine wewe unaweza kuwa mmoja wapo?

Umekaa bendi moja kwa miaka sita na kuendelea, hujawahi kutunga hata wimbo mmoja, huna mchango wowote uliotukuka ndani ya bendi, hujaweka alama yako yoyote kwenye bendi zaidi ya sura yako. Wewe ni kiazi.

Upo kwenye bendi ambayo inakunyanyasa, inakudharau, inakunyanyapaa lakini huna mpango wa kuthubutu kuhama, sio kwasababu unaipenda sana bendi bali ni kwasababu huna uhakika wa kupata ‘namba’ kwenye bendi nyingine. Wewe ni kiazi.Sishawishi watu kuhama bendi zao, lakini wakati mwingine kuhama bendi ni chachu ya kuthibitisha thamani yako, ni njia ya kubaini umuhimu wako kule unapotoka na unakokwenda. Ukiogopa kukabili changamoto mpya wewe ni kiazi.

Kama uliwahi kuhama bendi kwa mbwembwe halafu kule ulikokwenda kukabuma, huku bendi yako ya zamani ikiendelea kubaki katika ubora ule ule halafu mwisho wa siku ukarejesha mpira kwa kipa na kuomba urudishwe kundini bila bakshishi yoyote ya usajili, bila mkataba, bila makubaliano ya mshahara, wewe ni kiazi.

Kuna wakati bendi ya Twanga Pepeta iliwahi kupunguza kazi wasanii wake kwa madai ya kiwango duni (viazi), mmoja wapo alikuwa mwimbaji Jumanne Seseme “J Four Sukari” ambaye pia husimama kama rapa.

Jamaa akaenda TOT Band, akalamba ajira yenye uhakika wa mshahara, akawa moja ya wasanii nguzo wa bendi hiyo, baada ya muda bendi yake ya zamani (Twanga) ikaanza kummendea, ikaona umuhimu wake, ikahisi pengo lake na sasa mara kwa mara wamekuwa wakiomba msaada wake ashiriki kwenye baadhi ya maonyesho yao pale bendi yake ya TOT inapokuwa haina kazi.

Ingawa katika waliopunguzwa Twanga Pepeta wako walioshindwa kuthibitisha kuwa wao si viazi, lakini J Four ni mmoja wa wasanii waliofanikiwa kujisafisha, alipigwa panga Twanga lakini hakukata tamaa, akadhihirisha kuwa kuna maisha nje ya Twanga Pepeta na mwisho wa siku waliomuona kiazi wabeaini kuwa ni nyama.

Unamiliki bendi lakini unaona aibu kutaja kiingilio katika matangazo ya maonyesho ya bendi yako, unahisi kuwa kiingilio kile ni cha chini sana kuliko hadhi ya bendi yako, lakini bado unashindwa kujikwamua ili uondokane na hali hiyo, basi mmiliki wewe ni kiazi.

Naam hiyo ni mifano michache tu ya viazi ndani ya soko la muziki wetu, si jambo baya kuwa kiazi ila mbaya ni ile hali ya mtu kujitambua kuwa ni kiazi, ukishindwa kujitambua uko fungu gani basi kujinasua huwa ni mtihani.

Bendi zetu zinapigana vikumbo kwa wamikili wa bar zikigombea nafasi ya kufanya show kwa kiingilio kinywaji, zinaporomosha bei zao kwa ujinga, kwa fikra za kukomoana, matokeo yake zinaondoka na malipo kati ya shilingi laki mbili hadi saba, kundi lina zaidi ya watu 20 linagawana vipi malipo hayo? Huu ni u-kiazi uliopitiliza.

No comments