AZAM FC YAACHANA NA MGHANA YAHYA MOHAMMED

PINGU iliyofungwa na klabu ya Azam FC na Mghana Yahya Mohammed imevunjika rasmi baada ya pande zote mbili kumalizana mezani.

Afisa habari wa Azam, Jaffar Idd Maganga amesema kwamba klabu imeachana na mchezaji huyo rasta baada ya kutoridhishwa na uwajibikaji wake kwenye timu.

“Tulikaa mezani tukakubaliana kuachana kwa amani baada ya sisi kama klabu kutoridhishwa na mchango wake kwetu, hivyo kuanzia sasa yuko huru,”amesema Jaffar.

Nyota huyo alisajiliwa Azam kwa matarajio makubwa mwezi Juni mwaka jana kwa dau la dola za Kimarekani, 100,000 zaidi ya sh. Mil 220 kutoka Aduana Stars ya kwao.

Ni moja kati ya wachezaji watano wa Ghana waliosajiliwa Azam FC wakati huo wengine ni Daniel Amoah, Enoch Atta Agyei Medema SC, Samuel Afful kutoka Sekondi Hasaacas na Yukubu Mohammed kutoka Aduana Stars  pia.

Mwanzoni mwa msimu, Azam ilimtema Afful na kumsajili kipa Mghana pia, Razak Abaslora kutoka klabu ya Wafa ya kwao.


Jaffar amesema baada ya kuondolewa na Yahya kocha Mromania Aristica Cioaba amepewa jukumu la kumsajili mshambuliaji mwingine.

No comments