DONALD NGOMA AZIDI KUWA "PASUA KICHWA" YANGA SC

MSHAMBULIAJI wa timu ya Yanga, Donald Ngoma ameacha kiza kinene Jangwani kufuatia kuendelea na msimamo wake wa kutowasiliana na uongozi wa klabu tangu alipoenda kwao Zimbabwe.

Mshambuliaji huyo alipewa kibali cha kwenda kwao kupumzika huku akijiuguza jeraha lake la goti ambalo limekuwa likimsumbua tangu msimu uliopita lakini mpaka hivi sasa hakuna mawasiliano yoyote kati yake na klabu.

Kwa mujibu wa kibali alichopewa, alipaswa kuwa amesharejea lakini hakufanya hivyo na kama kwamba haitoshi, ameendelea kuwa kimya mpaka leo.

Taarifa kutoka vyanzo vya ndani vimethibitisha juu ya hali hiyo na kudai kuwa uongozi utatangaza msimamo wake hivi karibuni ikiwa hali hiii itaendelea.

Yanga iko kwenye mchakato wa kusaka mchezaji mwingine wa kimataifa ili kukiongezea nguvu kikosi chake katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika sambamba na kutetea taji la Ligi Kuu bara.

Ngoma raia wa Zimbabwe alianza vyema kwenye kikosi cha Yanga wakati anasajiliwa na kuwa miongoni mwa wachezaji muhimu lakini tangu apate jeraha la goti amekuwa haeleweki.

Kabla ya kuanza kwa msimu huu alienda nchini Afrika Kusini kupatiwa matibabu alipomaliza akapewa mkataba mpya lakini bado hajaweza kurejea kwenye kiwango chake cha zamani.


Kuna hatari jina lake likawa miongoni mwa nyota watakaotemwa mwishoni mwa dirisha hili la usajili ili kuipunguzia klabu mzigo wa kulipa mishahara hewa.

No comments