HAKUNA KUREMBA!! MOURINHO AMCHINJIA BAHARINI LUKAKU KWENYE PENALTI DHIDI YA BENFICA


JOSE MOURINHO amesema straika wake mwenye thamani ya pauni milioni 75, Romelu Lukaku, atamruhusu kupiga penati pale tu watakapokuwa wamejihakikishia ushindi.

Wakati Anthony Martial akiwa amekosa penati kipindi cha kwanza Jumanne usiku dhidi ya Benfica, Lukaku alichukua mpira kwenda kupiga penati nyingine iliyopatikana kipindi cha pili, lakini Mourinho aliingilia na kutaka Daley Blind apige, na akafanikiwa kuiweka mbele United kwa mabao 2-0.

Alipoulizwa na Viasport Fotball kwanini hakutaka Lukaku kupiga penati, Mourinho alieleza: “Kwa sababu mimi ni kocha na ninafanya uamuzi. Alikosa penalti yake ya mwisho, nataka apige penalti wakati hakuna presha, wakati hakuna jukumu, na wakati hakuna haja ya kufunga.

“Tunacheza katika Ligi ya Mabingwa, tunahitaji pointi... Ilikuwa wakati muhimu wa mchezo, zikibaki dakika 10 kumalizika. Nataka mchezaji asiye na presha ya kuwa alikosa penati iliyopita.

 “Ninafurahi kwamba anataka kuchukua jukumu, lakini niko hapa wakati mwingine kulinda wachezaji na kulinda timu... Na labda Blind angekosa, lakini ninahitaji kumlinda (Lukaku) kwa sababu amepoteza penati ya mwisho.”


Mourinho aliongeza: “Nadhani nimemlinda. Kwa sababu kama angekosa penati, timu ingekuwa katika hatari.” Alikuwa akimaanisha kuwa uongozi wa bao 1-0 ulikuwa bado haujawahakikishia ushindi wakati kukiwa na dakika kumi mbele.

No comments