HANS PLUIJIM AANZA KUTEMBEZA "SHOKA" SINGIDA UNITED

BAADA ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Lipuli FC, kocha wa Singida United, Hans Pluijim ameanza kutembeza panga la usajili kwa kikosi chake.

Pamoja na kuwa na idadi ndogo ya mabao, timu hiyo ngeni Ligi Kuu haijaruhusu wavu wake kuguswa kwa mechi saba za Ligi Kuu Bara ambapo kocha huyo amekuwa akitumia mfumo wa soka la kujihami.

Klabu ya Singida United imekubali kumtoa kwa mkopo mshambuliaji wake Pastory Athanas kwenda Stand United baada ya straika huyo wa zamani wa Simba kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza.

Kocha Hans van der Pluijim amesema kwamba ni kweli wamemtoa kwa mkopo mchezaji huyo huku pia akijaribu kuangalia nyota wengine wa kuwaacha ili kupisha nafasi ya wachezaji wapya msimu huu.

“Ni kweli nimemruhusu Pastory kwenda Stand United kwa mkopo wa miezi sita ili akapandishe kiwango chake, lakini pia natazamia kuangalia wengine wa kuachana nao ili kupisha ingizo jipya la wachezaji,” alisema Pluijim.


Pluijim alisema anataka kusajili wachezaji wachache ambao watakiongezea nguvu kikosi chake na kutimiza dhamira yake ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya kwanza msimu huu.

No comments