HAPATOSHI UZINDUZI WA ALBAMU YA MJENGONI CLASSIC BAND YA ARUSHA


WAKATI tarehe rasmi ya uzinduzi wa albamu yao ‘Tunatosheka na afadhali’ ikiwa imetajwa, Bendi ya Mjengoni Classic ‘wakali wa–City’ wako kambini kwa mazoezi makali kujiandaa na uzinduzi huo.

Rais wa bendi hiyo Digitale Mukongya ‘Tiger’ amesema wako kwenye mazoezi makali kwa ajili ya staili mpya za uchezaji lakini pia kuhakikisha wanakuwa tofauti katika usiku huo. Albamu hiyo itazinduliwa Novemba 25, katika ukumbi wao uitwao Mjengoni, Olasite, Arusha ikiwa na nyimbo sita.

“Mambo yote yanakwenda vizuri…sie Tunatosheka na Afadhali, kutakuwa na dance mpya, mavazi mapya, sound mpya hata setup ya ukumbi itakuwa tofauti na siku zote, wapenzi wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia na kifedha,” alisema.

Digitale alisema mpaka sasa wanakamilisha mikataba na wasanii watatu wakubwa ambao watasindikiza albamu hiyo ambayo imefanyika kwenye studio tofauti mjini Dar es Salaam.

“Kila kitu kinakwenda sawa, tutawatangaza wasanii watakaosindikiza uzinduzi wa albamu hiyo lakini pia sherehe zetu za kutimiza mwaka mmoja…bendi nyingi hazifikishi hata miezi miwili utasikia wamepigana mara ugomvi lakini sisi mwaka sasa ni jambo la kumshukuru Mungu.”

Bendi hiyo ina nyota wengine kadhaa waliowahi kutamba na makundi mbalimbali nchini. Katika kikosi hicho yupo Donal Mikembe au Donaa Zinganguvu ‘Chokoraa’ ambaye alitamba kwenye kibao cha Bana Beta chao Beta Musica, yupo repa Yanike Noah ambaye alitamba Diamond Musia kabla ya kwenda Mashujaa Musica.

Yupo pia mpiga solo Sele Mumba ambaye alipita African Stars ‘Twanga Pepeta’ kabla ya kwenda Double M kwa Muumin Mwinjuma na mwanadada Princess Jean ambaye alitamba na Waluguru Original ya Morogoro.

No comments