HASSAN KESSY AKIRI NGOMA NZITO KWA YANGA LIGI KUU BARA MSIMU HUU

BEKI wa kulia wa timu ya Yanga, Hassan Ramadhani Kessy ambaye alitua kwenye kikosi hicho akitokea Simba amesema kwamba ni kweli msimu huu wamekuwa na upinzani mkali kwasababu timu nyingi zinacheza soka la kukamilika lakini dhamira ya kubeba ubingwa haiwezi kufutika.

Beki huyo anayewania namba ya Juma Abdul amedai kuwa mwenendo wao kwenye msimamo wa Ligi hauna mashaka sana isipokuwa amekiri kupata upinzani mkali na hasa wanapocheza mechi na timu za mikoani.

“Ni kweli Ligi ipo kwenye mzunguko wa tisa lakini mpaka sasa hakuna timu inayoweza kujihakikishia ubingwa kwasababu hata alama tulizotofautiana si nyingi ndiyo maana naona bado tuna nafasi ya kufanya kitu msimu huu,” alisema beki huyo.

“Ukipoteza mechi moja tu tayari aliyekuwa chini yako anakuvuka, hesabu za ubingwa msimu huu ni ngumu kuliko msimu uliopita lakini nafasi tuliyopo inaonyesha wazi tunawania taji linguine,” aliongeza.

“Lakini ndio uzuri wa Ligi yenyewe, timu nyingi zimesajili vizuri."

"Kama ilivyo kwa Singida United ambao wamejaza wachezaji wengi wenye uzoefu na michuano mikubwa,” alimaliza.

Yanga ambao ni mabingwa mara tatu mfululizo wa Michuano ya Ligi wanatarajia kushuka uwanjani Novemba 19 kucheza dhidi ya Mbeya City katika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam.

Timu hizo zinakutana huku Yanga ikiwa na kumbukumbu ya kupata sare ya bila kufungana kwenye mchezo dhidi ya Singida United wakati Mbeya City wao walifungwa 1-0 na Simba bao ambalo lilizua utata kwa kile kilichodaiwa kuwa mfungaji Shiza Kichuya alikuwa ameotea.


Hivi sasa kikosi cha Lwandamina kimejikusanyia jumla ya alama 17, baada ya kucheza mechi tisa huku wapinzani wao wakubwa Simba na Azam FC wakiwa na pointi 19.

No comments