HUMUD AFUNGUKA KISA CHA KUITEMA MAJIMAJI

KIUNGO Abdulhalim Humud amefunguka kilichosababisha aiteme timu ya Majimaji baada ya kuandika barua ya kuomba kusitisha mkataba wake na klabu hiyo ya mkoani Songea.

Humud ambaye amewahi kuzichezea timu za Simba, Azam, Costal Union na Mtibwa, aliandika barua ya kuomba kutemwa kwenye kikosi hicho ambayo ilipokelewa kwa mikono miwili.

Klabu ya Majimaji haikuweka wazi sababu iliyopelekea nyota huyo wa zamani wa Taifa Stars kuondoka kwenye kikosi chao wakati huo Ligi ikiwa inaendelea katika mzunguuko wa nane.

“Niliporudi Afrika Kusini nilitaka kucheza nyumbani bila kuchagua ukumbwa wa timu, nilitazama kwanza maslahi kwasababu nilikuwa na malengo yangu ya kucheza walau nusu msimu kabla ya kuamua jambo lingine,” alisema Humud.

“Tulikubaliana vizuri kuhusiana na masuala ya hela ya usajili na mshahara lakini kuna changamoto ambazo zilijitokeza katikati nikaamua kujiweka pembeni, lakini sina lawama kwa kiongozi yeyote,” alisema.

“Nashukuru hata wao viongozi wa Majimaji wamekuwa waungwana katika suala hili, ilipofika hatua ya kusitisha mkataba wala hawakuwa na kinyongo, tulimalizana kwa amani tu,” aliongeza mchezaji huyo.


“Kazi yangu ni mpira na wala sina mashaka kuwa nitaendelea kuonekana uwanjani bila kujalisha ni wapi.”

No comments