ISHU YA KUBEBWA NA KITUO CHA RADIO: HAYA NDIYO MAJIBU YA CHRISTIAN BELLA


Mwimbaji nyota wa dansi Christian Bella, amepinga hoja kubebwa na kituo cha radio iliyotolewa na mwimbaji nguli Mwinjuma Muumin.

Hivi karibuni, Muumin akionngea na kituo cha 98.5 AM FM Radio, alisema Bella yuko juu kwa kuwa anabebwa na kituo kimoja cha radio kwa maslahi yao binafsi.

Muumin alinukuliwa na Saluti5 akisema kupitia kituo hicho: “Muziki wa dansi uko chini kwasababu vituo vya radio vimegeemea kwenye bongo fleva, singeli na taarab.

“Sasa hivi mtu wa dansi ambaye yuko juu ni Christian Bella na hiyo ni kwasababu kuna kituo cha radio kina mbeba kwaajili ya maslahi yao binafisi.

“Bella anabebwa, lakini kiukweli kabisa leo umsimamishe Bella na Muumin halafu uwaambie wapige muziki wa kweli, anaweza akakimbia mtu hapo”.

Lakini Jumamosi usiku kipindi cha Weekend Bonanza cha Clouds FM, kikaamua kumchokonoa Bella juu ya madai hayo ya Muumin na kuhusu pia ni nani zaidi kati yake yeye na Muumin.

Mtangazaji wa kipindi hicho cha Weekend Bonanza, Khamis Dacota akasoma ujumbe wa Christian Bella uliojibu madai ya Mwinjuma Muumin kama ifuatavyo: “Kuhusu nani mkali kati yangu na Muumin, binafsi naona Muumin yuko juu, kanizidi kwa kila kitu na kamwe siwezi kushindana nae.

“Kuhusu ishu ya kubebwa, si kweli bali ni ubora wa kazi zangu ndio unaofanya niwe juu kiasi cha wengine kuamini kuwa nabebwa.

“Nimetoka kwetu Congo kuja Tanzania kwaajili ya kutafuta pesa kupitia muziki. Najitahidi kulisoma soko kila siku na kubadilika kadri ya mahitaji ya soko yalivyo.

“Kadri soko linavyobadilika ndivyo ninavyoona kuwa hiyo ni fursa mpya kwangu ya kupiga hatua nyingine, naangalia soko linahitaji nini na sio kile ninachohitaji mimi. Hiyo ndiyo inayofanya hata baadhi ya watu wanilinganishe na nyota wa bongo fleva kama kina Diamond na Ali Kiba.

“Kwa kuwa Muumin ni mkali na anakubalika zaidi kama anavyoamini, basi naomba atumie ukocha na ugwiji wake kuipandisha juu bendi yake na muziki wa dansi kwa ujumla”.

No comments