LICHA YA KUSAJILIWA BURE, SEAD KOLASINAC AGEUKA LULU ARSENAL


SEAD KOLASINAC amekuwa na mwanzo mzuri wa maisha Arsenal, kiasi cha kupagawisha mashabiki na zaidi straika Alexis Sanchez ambaye amefunguka kuwa hata wakiwa mazoezini, anapenda zaidi kucheza naye kikosi kimoja kuliko kuwa vikosi tofauti.

Raia huyo wa Bosnia mwenye umri wa miaka 24, aliyetua Emirates kwa usajili huru akitokea Schalke majira ya kiangazi, aling’ara wikiendi iliyopita baada ya kufunga bao la kusawazisha dhidi ya Swansea, kabla kutengeneza bao la ushindi lililofungwa na Aaron Ramsey.

 "Ni vigumu [kucheza dhidi yake mazoezini], kwa sababu ana nguvu na ni vigumu kumtoka!" alisema Alexis akizungumza na tovuti rasmi ya Arsenal.

"Yeye ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa na ana nguvu sana... Anatengeneza pasi nzuri, hivyo naweza kufunga. Ni mchezaji mwenye akili, ambaye anaweza kutengeneza nafasi nzuri za kufunga.

"Tayari ameonyesha ubora wake. Amefunga mabao, ametengeneza nafasi na kuonyesha kile anachoweza kufanya katika michezo ya Ulaya na ligi. "

No comments