LIPULI YAKANA KUWATEMA JUMLA MACHAKU NA MALIMI BUSUNGU

KLABU ya Lipuli FC ambayo ilitangaza kuwasimamisha wakongwe wake wawili Salum Machaku na Malimi Busungu kwa muda usiojulikana, imetoa taarifa ya kukanusha kuwatema nyota hao wawili kikosini.

Lipuli ilitoa taarifa ya kuwasimamisha wachezaji hao kwa utovu wa nidhamu pasipo kueleza aina ya makosa waliyofanya lakini taarifa zilizozagaa ni kuwa wachezaji hao wamekuwa na tatizo la unywaji wa pombe uliokithiri.

Afisa habari wa klabu hiyo, Clement Sanga amethibitisha kuwa ni kweli wachezaji hao wamesimamishwa kwasababu ya kurudia kosa moja mara kwa mara lakini alikanusha vikali suala la kuwatema kikosini.

“Ni kweli wachezaji hawa wamesimamishwa ili kuona ni kwanini wamekuwa wakirudia kosa moja mara kwa mara lakini suala la kuwatema kikosini halina ukweli wowote kwasababu wana mikataba halali na klabu,” alisema afisa habari huyo.

“Suala lao lipo kwenye kamati ya nidhamu na linaendelea kujadiliwa na muda ukifika tutaweka wazi kila kitu ila kwa wakati huu bado wanaendelea kutumikia adhabu waliopewa,” aliongeza.


Malimi Busungu amewahi kutamba akiwa na kikosi cha timu ya Yanga wakati Salum Machaku yeye aliwahi kuchezea Simba miaka ya nyuma kabla ya kutemwa.

No comments