LWANDAMINA, TSHISHIMBI WAIPASUA KICHWA SIMBA SC

VIGOGO wa Simba inasemekana bado wanakuna vichwa juu ya makali ya uwezo wa Yanga lakini walichoshitukia sasa ni kwamba uwezo wa kocha George Lwandamina sio kitu kinachotakiwa kupuuzwa.

Kigogo mmoja wa Simba amefunguka kwamba sio kitu cha kuficha kwamba Lwandamina ni kocha anayejua kuwasoma wapinzani na kutengeneza mpango wa kuwazuia.

Bosi huyo alisema ubora wa kocha huyo ni kitu kikubwa kinachoipa makali Yanga huku pia akisifia usajili wa mchezaji wa timu hiyo, Papy Kabamba Tshishimbi kuwa ni ingizo bora.

Alisema bado wanaumiza kichwa jinsi kuidhibiti Yanga hasa makali yao hayo lakini pia wanajipanga kufanyia maboresho timu yao kwa kuwatimua wachezaji mizigo.

“Tunaifuatilia Yanga na kikubwa tu ninachokiona katika timu yao ni uwezo wa kocha wao, huyu ni mtu hatari sana. Ukiangalia kila mchezo anaocheza anakuwa na mipango ya akili nyingi sana,” alisema bosi huyo.


“Ukiangalia hata katika mchezo wetu alitubana sana, kiukweli hatukuweza kuimiliki Yanga. Angalia mashambulizi yake yalivyokuwa ya hatari lakini pia hata huyu Tshishimbi naye ni mtu anayechangia.”

No comments