MBEYA CITY YASHIKILIA ROHO YA JOSEPH OMOG

TIMU ya Mbeya City imetamba kuwa hawataiacha Simba salama katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania bara ambao utachezwa kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.

Kama ndoto hiyo itatimia basi kibarua cha kocha wa Simba, Joseph Omog raia wa Cameroon kitakuwa hatarini.

Habari kutoka ndani ya klabu ya Simba zinadai kuwa mechi hiyo ni moja ya kipimo kitakachohalalisha kuwepo au kutokuendelea kwa Omog kukalia benchi la ufundi.

Simba walipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga na hivi sasa wanatarajiwa kuwa wageni wa Mbeya City Jumapili ya wiki hii.

Meneja wa Mbeya City, Geoffrey Katepa amesema kwamba hawawezi kukubali kuendelea kupoteza mechi baada ya kufungwa na Azam FC kwa bao 1-0 katika mchezo uliopita.

“Dar es Salaam tulipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Azam hivyo lazima tuhakikishe Simba wanaziacha alama zote tatu ugenini ili tuendelee kubaki kuwa salama,” alisema meneja huyo.

“Siwezi kusema Simba hawana kikosi kizuri kwasababu tumewaona walivyocheza na Yanga Jumamosi, lakini kwetu mpango namba moja ni kuchukua alama tatu dhidi yao,” aliongeza.

Timu ya Mbeya City ambayo iko chini ya kocha mpya, inakamata nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na jumla ya alama 11 ilizozipata baada ya kucheza michezo yake nane ya mzunguuko wa kwanza.

Wakati huohuo, klabu ya Simba ina jumla ya alama 16 ikilingana na timu za Yanga, Azam FC na Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro.

Jumamosi ya wiki hii pia kutakuwa na mechi nyingine kali ambapo Kagera Sugar watacheza dhidi ya Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Kaitaba, Bukoba, huku Njombe Mji FC wakiwa wenyeji wa Mbao FC katika dimba la Sabasaba na Azam FC watacheza dhidi ya Ruvu Shooting.

No comments