MSUVA ATABIRI UBINGWA WA CECAFA UTATUA KILIMANJARO STARS

WINGA wa kimataifa wa timu ya Difaa El Jadida ya nchini Morocco, Simon Msuva amesema kuwa haoni sababu itakayoifanya Kilimanjaro Stars ishindwe kubeba ubingwa wa Kombe la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Challenge), kutokana na aina ya kikosi ambacho kimeitwa.

Kilimanjaro Stars itafungua dimba na Libya Desemba 3, mwaka huu, mchezo ambao utafuatiwa na mechi kati ya wenyeji, Kenya dhidi ya Rwanda.

Baada ya mechi hiyo, itarudi tena dimbani Desemba 7, kucheza dhidi ya Zanzibar Heroes kisha Desemba 9 itakumbana na Rwanda kabla ya kumaliza mechi zake za Kundi A kwa kucheza dhidi ya wenyeji Kenya Desemba 11.

Msuva amempongeza kocha Ammy Ninje kwa uteuzi mzuri wa kikosi chake huku akidai kuwa kuna kila dalili ya kuleta Kombe nyumbani kutokana na uzoefu wa mastaa watakaosafiri na timu.

“Ni kikosi chenye mseto wa wachezaji walioko kwenye viwango, mtu kama Danny Lyanga hapo kabla hakuwahi kuitwa lakini ni mchezaji mwenye shauku ya mafanikio, nafikiri kuna kitu kizuri kinakuja Kilimanjaro Stars,” alisema Msuva.

“Ni zamu ya Kilimanjaro Stars kufanya vyema. Sioni kama kuna uwezekano wa kurudi mikono mitupu katika michuano hii,” aliongeza winga huyo wa zamani wa Yanga.

Kikosi kilichoitwa ni pamoja na makipa Aishi Salum Manula, Peter Manyika huku mabeki wakiwa ni Boniface Maganga, Gabriel Michael, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein na Kenned Wilson.


Viungo ni Himid Mao, Hamis Abdallah, Raphael Daudi, Ibrahim Ajib, Muzamil Yassin, Jonas Mkude, Shiza Kichuya na Abdul Hilal, wakati washambuliaji ni Mbaraka Yusuph, Daniel LyangaElias Maguri na Yohanna Mkomola.

No comments