MTIBWA SUGAR SWAAFI... yarejea Manungu kutoka Lindi full burudani

TIMU ya Mtibwa Sukari imeondoka mkoani Lindi na kurejea Turiani Morogoro ikiwa na hali ya utulivu baada ya kushinda mechi zake mbili mfululizo za kirafiki mkoani humo na sasa hesabu zao wamezielekeza kwenye mchezo dhidi ya ndugu zao, Kagera Sukari.

Mtibwa inatarajia kuwa wenyeji wa Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu itakayochezwa Novemba 18, mwaka huu katika uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

Katibu msaidizi wa klabu hiyo, Abubakar Swabur amesema kwamba baada ya ziara hiyo yenye mafanikio, hivi sasa akili yao wameielekeza kwenye mchezo huo utakaopigwa Manungu.

“Tumemaliza ziara salama kwa ushindi mnono. Hii inatupa picha nzuri katika mchezo wetu unaofuata kwa sababu tutakuwa katika uwanja wa nyumbani na tunapaswa kushinda kwa kila namna,” alisema kiongozi huyo.

Mtibwa ilipokuwa Lindi ilicheza mechi za kirafiki dhidi ya Monaco na kushinda kwa mabao  5-0 kisha ikaifunga Black Mob 3-1.


Mchezo wao wa mwisho dhidi ya Ndanda FC walipata sare ya 0-0 lakini hata hivyo haijawaondoa kwenye mbio za ubingwa wakiwa wameachwa kwa alama mbili tu na vinara Simba ambao walishinda bao 1-0 dhidi ya Mbeya City.

No comments