MTIBWA SUGAR WAFARIJIKA KUWA SAWA NA YANGA MSIMAMO LIGI KUU BARA

BAADA ya kupata sare na Ndanda FC, kocha wa timu ya Mtibwa, Zuberi Katwila amesema kuwa anashukuru walau kuambulia alama moja na kuendelea kulingana na Yanga katika msimamo wa Ligi huku wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa tu.

Mchezo wa Mtibwa Sugar na Ndanda FC ulichezwa juzi katika uwanja wa Nangwanda Sijaona na kumalizika kwa sare ya bila kufungana.

“Ligi imekuwa ngumu msimu huu tofauti na mwaka jana, nashukuru walau kwa kuambulia alama moja ugenini kwasababu bado hatujapoteza uelekeo wa kubeba ubingwa,” alisema kocha huyo.

“Wapinzani wetu sio wa kuwabeza na ukizingatia kwamba walikuwa katika ardhi ya nyumbani na mashabiki wengi, hivyo ninashukuru hata kwa hiki tulichovuna kuliko kupoteza mchezo kabisa,” alimaliza.

Timu ya Mtibwa Sugar imeendelea kulingana na Yanga baada ya kucheza michezo tisa na kujikusanyia jumla ya alama 17.
Kabla ya mechi za wikiendi kulikuwa na timu nne zilizokuwa na alama sawa ambazo ni Azam FC, Simba, Yanga na Mtibwa Sukari.


Lakini ushindi wa juzi wa Azam FC dhidi ya Ruvu Shooting unaifanya timu hiyo kusimama juu ya timu za Yanga na Mtibwa ambazo ziliambulia sare.

No comments