MUUMIN: ‘SIJAONEKANA’ KWENYE TV TANGU SHAMBA LA BIBI MWAKA 2013


Umewahi kuhisi sababu zinazopelekea muziki wa kizazi kipya kuwa juu? Mojawapo ni video, vijana wengi wa bongo fleva hawakubali kuachia nyimbo bila video.

Umewahi kuhisi moja ya sababu zinazoporomosha muziki wa dansi? Ni video, wasanii wa dansi wanachukua muda mrefu kuachia video mpya. Jiulize tu lini mara ya mwisho kuona video mpya ya Twanga Pepeta, Msondo, Sikinde, Vijana Jazz, Ivory Band, Talent Band na nyingine nyingi.

Mmiliki wa Double M Plus, Mwinyuma Muumin amekiri kuwa hajaonekana kwenye TV akiwa na nyimbo mpya tangu mwaka 2013 alipotoa video ya “Shamba la Bibi” kupitia Victoria Sound. Miaka minne bila video mpya.

Akiongea na kituo cha 98.5 AM FM Radio cha jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Muumin akasema sasa yuko mbioni kutengeneza video mpya kwa vile ni muda mrefu hajaonekana kwenye TV akiwa na nyimbo mpya.

“Tangu mwaka 2013, nilipotoa “Shamba la Bibi” sijatoa video nyingine, sasa nataka niachie video mpya isambae mitandaoni na kwenye vituo vya televisheni ili kuongeza soko langu,” alisema Muumin.

Kuthibitisha hilo, Muumin ameiambia Saluti5 kuwa uchukuaji wa video ya wimbo “Mwanzo wa Mafanikio” umekamilika na kwamba muda si mrefu kichupa kipya kitakuwa hewani.

No comments