OMOG APINGA MADAI YA KUIPONDA SAFU YAKE YA ULINZI

KOCHA wa Simba, Joseph Omog raia wa Cameroon amegeuka mbogo kufuatia madai ya kukiponda kikosi chake kuwa na safu mbovu ya ulinzi inayoruhusu mabao kizembe katika mechi za Ligi Kuu bara.

Mashabiki wa kikosi cha Simba wamekuwa wakihoji mitandaoni kufuatia mwenendo wa safu yao ya ulinzi ambayo iliruhusu bao kizembe kwenye mchezo dhidi ya Yanga uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mwanjali hakumkaba vyema Ajib na kutoa pasi kwa Mwashiuya ambaye pia hakuwa amekabwa akapiga pasi kwa Chirwa akiwa anaangaliwa na Juuko pamoja na Zimbwe Jr akafunga kwa urahisi.

“Ni kweli katika mchezo uliopita tulipoteza umakini tukaruhusu bao kizembe, lakini hiyo haina maana kuwa Simba ina safu mbovu ya ulinzi,” alisema Omog.

“Mechi za Simba na Yanga zina upekee wa aina yake na mara nyingi zimekuwa ngumu kwa kila upande hivyo sioni haja ya kuilaumu safu ya ulinzi.”


Simba inashutumiwa kuruhusu bao kizembe huku wakiwa na mchezo mgumu ugenini katika uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya ambapo watakwaana na wenyeji Mbeya City FC waliopania kuwazuia.

No comments