PRISONS YAFUKUZA MWIZI KIMYAKIMYA LIGI KUU TANZANIA BARA

TIMU ya Tanzania Prisons ya Mbeya haipewi nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara lakini kwa mwenendo wa mechi zake za hivi karibuni na alama walizojikusanyia ni kama wananyatia ubingwa kimyakimya.

Juzi Prinsons walifanikiwa kuwafunga Ruvu Shooting kwa bao 1-0 katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Sokoine mjini Mbeya kupitia bao lililowekwa wavuni na Mohammed Rashid dakika ya 19.

Bao la Mohammed Rashid linawafanya kufikisha alama 13 ambazo ni sawa na timu ya Singida United, huku wakiwa wameachwa alama tatu na vinara wa Ligi, Simba, Yanga, Azam na Mtibwa Sugar wenye pointi 16 kila mmoja.

Lakini pia mfungaji wao pamoja na kutozungumzwa sana ameshafikisha idadi ya mabao matano sawa na mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajib huku wakimfukuzia kwa karibu staa wa Simba, Emmanuel Okwi mwenye mabao nane.

Kwenye msimamo, Prisons wanaonekana wapo nafasi ya tano lakini kwa pointi hawapo mbali na timu nne za juu zinazowania ubingwa Tanzania Bara.


Ligi Kuu itaendelea tena kesho Ijumaa ambapo Majimaji FC watakuwa wenyeji wa Stand United.

No comments