ROMELU LUKAKU ASEMA AKIUNGANISHA NGUVU NA IBRAHIMOVIC MBONA PATANOGA MANCHESTER UNITED


STRAIKA wa Manchester United, Romelu Lukaku, amesisitiza kuwa kurejea kwa staa mwenzake, Zlatan Ibrahimovic, kutawaongezea nguvu katika mbio za kuwania ubingwa Ligi Kuu England.

Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 36, hajacheza hata dakika moja kwenye kikosi hicho cha Mashetani Wekundu tangu asaini mkataba mpya majira ya joto, kwani bado anauguza majeraha yake ya goti aliyoyapata  Aprili mwaka huu.

Ibrahimovic ambaye aliongoza kwenye orodha ya mabao Man United katika kampeni yake ya kwanza Old Trafford, anatarajiwa kurudi dimbani kabla ya mwisho wa mwaka.

Alipoulizwa kuhusu mchango anaoutarajia kutoka kwa mchezaji mwenzake huyo, Lukaku aliiambia Sky Sport News: "Kurudi kwa Ibrahimovic kutatusaidia kuifukuzia Manchester City.

"Timu kama yetu ni ngumu sana kwa timu pinzani. Inanihamasisha kwa kweli, kwa sababu ni mchezaji mwingine bora sana atakayeongeza nguvu kikosini mwetu."

No comments