RONALDINHO ASEMA SOKA LA COUTINHO NI LA BARCELONA, SIO LIVERPOOL


Ronaldinho anaamini kiungo mshambuliaji wa Liverpool Philippe Coutinho atazoa mafanikio mengi Barcelona iwapo ataamua kuondoka Anfield na kwenda Nou Camp.

Barcelona ilimtaka Coutinho kwa kila hali dirisha la usajili la kiangazi lakini ofa zake nne zikapigwa chini na Liverpool ikiwemo ile yenye thamani ya pauni 138.

Coutinho akaiomba timu yake ikubali kumuuza lakini Liverpool ikasimama imara na kusema hawapo tayari kufanya biashara kwa dau lolote lile.

Hata hivyo, Barcelona bado inamtaka nyota huyo wa kimataifa wa Brazil ambapo ripoti kutoka Hispania zinasema klabu hiyo itajaribu tena kumsajili Coutinho dirisha la Januari.

Ronaldinho, staa wa zamani wa Barcelona na Brazil anaunga mkono mpango huo kwa kusema aina ya uchezaji wa Coutinho inafiti zaidi Barcelona.

"Hakuna shaka kuwa uamuzi ni wa kwake mwenyewe Coutinho, lakini Barcelona ndiyo timu itakayomfaa zaidi" alisema Ronaldinho katika maongezi yake na gazeti la Mirror.
No comments