AMIS TAMBWE APONA MAJERAHA... kuanza na Ndanda Desemba 31

MSHAMBULIAJI wa timu ya Yanga, Amis Tambwe ambaye ameponea kwenye tundu la sindano baada ya kuhusishwa kutaka kuachwa, ametangazwa kuanza katika mchezo wa Ligi Kuu bara dhidi ya Ndanda, Desemba 31 mwaka huu.

Tambwe amekosekana uwanjani tangu kuanza kwa msimu huu kutokana na majeruhi, jambo lililochangia kutaka kutemwa kwenye kikosi hicho kinachotarajia kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Ofisa wa klabu ya Yanga, Dismas Ten amesema kwamba mshambuliaji huyo hana tatizo lolote la kiafya na tayari amejumuishwa katika program za kocha George Lwandamina.

“Nikuhakikishie, Tambwe yuko fiti na atatumika katika mechi za Ligi zinazofuata isipokuwa kamusoko bado anaendelea na matibabu yake huku akifanya mazoezi ya taratibu,” alisema Ten.

Tambwe alipata jeraha mwezi Agosti mwaka huu katika kambi ya Yanga kisiwani Pemba.

Yanga itashuka dimbaniDesemba 31, mwaka huu katika mchezo dhidi ya Ndanda huku mahasimu wao Simba wakitarajiwa kucheza Desemba 30.  

No comments