AMISSI TAMBWE AANZA KUJIPENDEKEZA KWA GEORGE LWANDAMINA

MSHAMBULIAJI wa timu ya Yanga, Amissi Tambwe raia wa Burundi ni kama ameanza kujipigia upatu ili aingizwe moja kwa moja kwenye kikosi cha George Lwandamina baada ya kupona majeraha yake aliyopata visiwani wakati wa maandalizi ya msimu mpya.

Tambwe amenukuliwa akisema kuwa yuko fiti asilimia zote na haioni sababu ya kuwekwa benchi kwa sababu shauku yake ya kucheza ni kubwa baada ya kukaa nje kwa muda mrefu akijiuguza.

Wakati Tambwe akionyesha shauku ya kutaka kuanzishwa kikosi cha kwanza, kinda Nkomolo hana presha baada ya kuhakikishiwa nafasi ya uhakika kuanza kucheza.

Lwandamina amesema kwamba amemfuatilia Yohana Nkomolo kwa muda mrefu na kubaini ni mchezaji mwenye msaada mkubwa katika kikosi chake.

Nkomolo amecheza Yanga mechi moja tu tena ya kirafiki dhidi ya timu ya Police Dar es Salaam lakini Lwandamina amedai kukoshwa na mwenendo wa kijana huyo kuanzia kwenye program za uwanjani hadi jimu.

“Ni kijana mdogo akili yake inafundishika, anakamata mambo haraka, ni mwepesi anaweza kutusaidia katika ratiba za mechi zinazofuata,”alisema Lwandamina.


Nkomolo alisajiliwa na Yanga kwenye dirisha dogo la usajili akiwa sambamba na beki Mkongomani Feston Kayembe.

No comments