AYA 15 ZA SAID MDOE: DARASA UKICHEMKA 'MUZIKI' UTAKUPELEKA DARASANI (MAKALA YA JANUARI 30, 2017)

Tarehe 30 Januari mwaka huu niliandika makala ya msanii Darasa ambayo leo hii nimejisikia hamu ya kuirudia kama ilivyo bila kupunguza wala kuongeza neno. Niliandika kama hivi:

Naweza kusema kuwa zari limemwangukia mdogo wangu Darasa, msanii wa siku nyingi kwenye muziki wa Kizazi Kipya, lakini aliyeibuka hivi karibuni tu na kupata mafanikio makubwa kupitia wimbo wake wa "Muziki".

Nina mengi ya kumuasa Darasa katika kipindi hiki ambacho anatesa na kibao hicho, hasa ikizingatiwa kuwa alishasota sana kwenye gemu akiwashuhudia wenzake wakitusua, lakini hakukata tamaa.

Tangu baada ya kuachiwa kwa wimbo " Muziki", zimeshatoka nyimbo nyingine nyingi za Bongofleva kutoka kwa wasanii wenye majina makubwa zaidi yake, lakini bado mashabiki huwaambii kitu kwenye kibao hicho - Hii ina maana nyingi lakini kubwa ni kuwa 'kila nabii na zama zake' - Kwamba kama Mungu kakuandikia kutusua, basi utatusua tu.

Kwa sababu wote tunafahamu kuwa Darasa si wa jana wala juzi kwenye muziki na ameshatoa nyimbo nyingi ambazo pengine nyingine ni kali kuliko "Muziki" lakini hazikubahatika kushika chati namna hii, basi kazi pekee kubwa iliyobaki kwa Darasa hivi sasa ni kuhakikisha analinda daraja alilopanda kwa ghafla bila mwenyewe kutarajia.

Anapaswa sasa kuumiza kichwa kwelikweli, asikurupuke na kuachia nyimbo zisizo na kiwango ambazo zinanaweza kumporomosha badala ya kumbakisha kileleni.

Wimbo huu wa “Muziki” unaweza kuwa ni ngazi ya kumpeleka Darasa kwenye kilele cha mafanikio, lakini unaweza pia kuwa ‘jeneza’ litakalomsindikiza kwenye safari ya kuzimika kimuziki iwapo atashindwa kuupiku yeye mwenyewe wimbo wake huo wa “Muziki”.

Muziki hauna mwenyewe hivyo lolote linaweza kutokea kwenye gemu kama hatokuwa makini, kwani nafasi aliyopo walishaishikilia wasanii wengi ambao hivi sasa wamebaki kugongea fegi tu vijiweni kwa kushindwa kujipanga ipasavyo.Kukubalika kwa wimbo "Muziki" kusimfanye abweteke kiasi cha kuona amemaliza kila kitu katika sanaa, akumbuke kuwa bado ana deni kubwa kwa mashabiki wake la kuhakikisha anafyatua ngoma kali zaidi kila anapozama studio kurekodi.

Kujisahau ni kati ya magonjwa mabaya mno yanayowafanya wasanii wetu wengi wasiweze kudumu kwenye chati kwa muda mrefu na ndo maana nasisitiza kumweleza kuwa nafasi aliyopo walishapita wengi.

Mashabiki ni wepesi wa kukusahau na kugeukia wengine wanaofanya vyema, hata kama nyimbo zako zilikuwa na uzuri wa namna gani ama ziliwafariji kwa kiwango kipi, hivyo hakikisha unawalinda na kuwazuia wasikukimbie.

Majuzi nilimsikia mmlikili wa Twanga Pepeta Mamaa Asha Baraka akimsifia radioni Darasa  na kukiri kuwa wimbo wa “Muziki” umeuteka nchini lakini akatoa angalizo kuwa msanii huyo sasa ana deni kubwa la kuhakikisha anatoa wimbo mkali zaidi vinginivyo atabakia kuwa historia.

Darasa anapaswa kuangalia mahitaji ya soko kwa wakati husika na asikurupuke kuachia wimbo mpya kwa kufuata mkumbo. Akae akijua kuwa kuna wasanii wengi waliopotea ghafla muda mfupi tu baada ya kutoa nyimbo kali zilizobeba heshima mithili ya wimbo wa taifa.

Anapaswa kuilinda kazi yake nzuri ambayo ni matunda yake ya ibada ya subira na moyo alionao wa wivu wa mafanikio na tamaa ya kufika pale ambapo wenzake wengine wanafika kila leo.

Hili pia liwe somo kwa wasanii hata wasio wa Bongofleva, maisha ya muziki yako hivyo na msifikiri kuwa kila mwaka utakuwa mwaka wako hata kama ni hodari wa kukesha ukitunga mistari.

Mwisho nimalizie tu kwa kusisitiza kuwa Darasa atake asitake, ni lazima atoe wimbo bora kuliko “Muziki” vinginevyo atajerejeshwa darasani.

No comments