HAJI MWINYI AKATAA KUKUTANA NA "WAPAMBE" WA FC LEOPARD

KUFUATIA taarifa za beki wa timu ya Yanga, Hiji Mwinyi kutakiwa na timu ya FC Leopard ya nchini Kenya, staa huyo wa Zanzibar Heroes amesema kuwa hana mpango wa kukutana na wawakilishi wa klabu hiyo kwa ajili ya kufanya mazungumzo.

Beki huyo alikuwa mhimili wa Zanzibar Heroes katika hatua ya fainali ya Chalenji dhidi ya Kenya ambapo alihusika na mabao yote mawili ya kusawazisha ambayo waliyapata kabla ya kuelekea hatua ya matuta ambapo Harambe Stars walishinda.

Mlinzi huyo wa kushoto amesema kuwa kama kweli FC Leopard wana nia ya dhati ya kutaka huduma yake inawabidi wakutane kwanza na viongozi wa klabu ya Yanga kbla ya kutaka mawasiliano nae.

“Hakuna wachezaji wanaokataa ofa kubwa lakini mimi ni mchezaji halali wa Yanga, bado nina mkataba Jangwani hivyo uongozi una mamlaka yote juu yangu siwezi kujiamulia tu,” alisema beki huyo.

“Leopard wanatakiwa kumalizana na viongozi wangu katika kipindi hiki cha mkataba na wakiona hawawezi kufanya hivyo basi wasubiri mpaka nitakapomaliza mkataba wangu na kuwa mchezaji huru,” aliongeza.


Hata hivyo, beki huyo amekuwa hapati namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza lakini kwa ratiba za George Lwandamina ambaye anakabiliwa na ratiba ngumu za michuano mingi anaweza asiruhusu kuondoka kwake.

No comments